KIONGOZI WA MADAKTARI NA DAKTARI BINGWA DK RODRICK KABANGILA AJIUNGA NA CHADEMA


Dk. Rodrick Kabangila aliyejiunga Chadema.
KIONGOZI WA MADAKTARI NA DAKTARI BINGWA AJIUNGA NA CHADEMA
 
PRESS RELEASE
Ndugu waandishi
Ndugu waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kufikisha miaka mitatu ya kuwatumikia Madaktari na Watanzania kwa ujumla kwa vile nimekuwa kiongozi wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) kwanza kama Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa miaka miwili na baadae Makamu wa Rais wa Chama hicho.
Kwa kupitia nafasi hizo za MAT nimeweza kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Kitaaluma vya Afya ambapo shirikisho hilo linajumuisha vyama vyote vya kitaaluma katika sekta ya afya. Nafasi nyingine muhimu ya kujivunia kuwatumikia Watanzania kitaaluma ni pamoja na kuwa katibu mkuu wa kwanza wa Chama Cha Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia Tanzania (TMDPWU) nikiwa mwanzilishi na kaimu katika nafasi hiyo.
Ndugu waandishi
Katika kipindi cha uongozi wangu nikishirikiana na wenzangu tumejitahidi kushiriki katika uboreshwaji wahuduma za afya Tanzania, na yafuatayo ni mfano;
1. Kushiriki katika kupitia Rasimu ya Sheria ya Madaktari ambayo itawezesha madaktari kufanya kazi kwa weledi zaidi na hivyo kupunguza makosa ya kitaaluma wakati wa utoaji wahuduma za afya. Rasimu hii iko katika hatua za mwisho za kwenda bungeni.
2. Kuandaa rasimu na kusajili chama cha Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia Tanzania ambacho kitajikita zaidi katika kudai maslahi huku kikiacha MAT kifanye kazi ya kuboresha taaluma. Chama hiki tayari kinaendelea kushamiri katika vituo vya kazi vya madaktari.
3. Kudai mazingira bora ya kazi katika sekta ya afya ikihusisha upatikanaji wa vifaa tiba na madawa kwa manufaa ya kuboresha hudumaza afya.
4. Kwa kushirikiana na SIKIKA kufanya utafiti uliowezesha kujua upungufu mkubwa wa madaktari katika utoaji wa huduma za afya. Utafiti huu utaiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi katika kushughulikia suala la Rasilimali watu katika afya.

Pamoja na haya yote mazuri niliyohusika katika kuongoza Madaktari na kuwa na moyo wa kuendelea kufanya hivyo, bado kuna mambo mengi hayaendi vizuri ambayo ni ya kimfumo katika serikali hii ya CCM ambayo yanaendelea kudidimiza huduma za afya. Mifano mizuri katika hili ni urasimu usio na maana katika usambazaji wa madawa na vifaa tiba, kutojali wataalamu, ufisadi na uzembe kauanzia wizarani, taasisi zake mfano Bohari la dawa mpaka katika vituo vya afya.
Ni kutokana na sababu hii inakuwa ngumu kwa vyama vya kitaaluma kuweza kuletama badiliko makubwa katika sekta hii na hivyo kuendelea kwa huduma duni za afya.
Naamini kuwa ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya katika jamii hii ya kitanzania kuna haja ya kubadilisha mfumo huu wa afya uliopo kwa kupata sera madhabuti zenye kujali Mtanzania maskini ambaye kwa kiasi kikubwa hawezi kumudu gharama za afya zinazopanda kila siku. Kwa hiyo mchango wa kisiasa ili kuwezesha haya unahitajika ili kubadilisha sekta hii ya afya Tanzania.

Ndugu waandishi
Ni kwa nia hii nzuri niliyo nayo na niliyoonyesha ya kuboresha sekta ya afya nchini ninafurahi kusema kuwa sasa ninahamishia rasmi nguvu zangu katika Chama cha siasa na hiki si kingine ni CHADEMA ambacho kimejipambanua kuwa chama cha watu kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Na kwa vile tayari nimeaminiwa kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya ZiwaMagharibiwa CHADEMA, nitatoa mchango wangu katika chama hicho ambacho nina hakika kitaweza kufikisha mazuri katika vyombo husika vya kimaamuzi mfano ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, halmashauri n.k.

Hivyo basi kwa kupitia sababu hii ya kuwa Kada rasmi wa CHADEMA bila kushurutishwa na kwa hiari yangu nang’atuka nafasi zangu zote za kuongoza Madaktari na watumishi wengine wa afya na tayari nimepata Baraka ya Halmashari kuu ya MAT ya kufanya hivyo kupitia kwa Rais wa Chama hicho;

Ndugu waandishi,
Nimeamua kufanya maamuzi haya ili
i) Kuondoa mgongano wa kimaslahi (conflicts of interests) kati ya Vyama ninavyoongooza, Madaktari, mimi mwenyewe na CHADEMA.
ii) Kuweza kuchangia kwa karibu zaidi katika Chama hiki kwa mawazo yangu ya kitaaluma ambayo nina hakika yatafanyiwa kazi na kuwa na manufaa zaidi katika uboreshaji wa sekta hii hasa wakati huu ambapo chama tayari kinaendelea kuandaa sera zake mbalimbali ikiwemo sera ya afya.
iii) Nikiwa kama msomi napenda kukiri waziwazi kuwa nitajishughulisha bila kificho katika kutoa mawazo na utaalamu wangu CHADEMA ili tuweze kwa pamoja kuwa na sera nzuri na kuboresha huduma za afya Tanzania.
iv) Kuwakumbusha watumishi wote wenye taaluma mbalimbali kuwa kushiriki katika harakati za kisiasa ili kuiondoa CCM si kosa la jinai kama ambavyo inataka kuaminishwa, na hii inajionyesha hata katika vifungu vya kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma;

• 5 (1) – Kinatoa haki ya kidemokrasia ya kuwa mwanachama wa Chama chochote.
• 5 (2) – Kushiriki masuala ya siasa lakini usionyeshe upendeleo wa kisiasa
• 5 (3) (a) – Usijuhusishe na siasa saa za kazi au mahala pa kazi

Ndugu waandishi
Napenda kuwashukuru Madaktari na watumishi wengine wa afya walioniamini na kunipa uongozi katika kipindi chote hiki na kuwa mimi bado ni mtaaluma na nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Vyama hivyo. Pia napenda kuupongeza nakuushukuru uongozi imara wa CHADEMA kwa kuniamini na kunipa nafasi ya mimi kushiriki katika mapambano haya ya ukombozi.
Mwisho kabisa, Napenda kuwasihi wataalamu wote wa chi hii kutokuwa waoga katika kujihusisha na mageuzi ya kiuchumi na kijamii ya nchi hii yanayoendelea na kwamba waache kulalamika tu bali wachukue hatua. Nchi hii ni yetu sote na sote tushiriki
kuijenga.

MUNGU IBARIKI TANZANIA
Dr. Rodrick Kabangila - Daktari bingwa wa Magonjwa ya Tiba, tafiti za huduma za afya na epidemiolojia
Mhadhiri Mwandamizi – CUHAS - Bugando
Makamu Mwenyekiti – CHADEMA Kanda yaziwa Magharibi


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...