Kulia ni Rhoda Mwakyusa(50), akifuatiwa na mwanaye Sabina Mwakyusa Mwafyela(28), mume wa Sabina na Dada yake Sabina kushoto.
Sabina Mwakyusa(28) anayedai alifukuzwa na manesi
wodini na kujifungulia nje ya geti usiku huku mvua ikinyesha akiwa na
Mama yake mzazi, Rhoda Mwakyusa(50).
Mtoto aliyezaliwa usiku nje ya geti la Hospitali ya Ifisi Mbalizi, baada ya mama yake kudaiwa kufukuzwa akiwa na uchungu.
*Walinzi wamsaidia.
Na Gordon Kalulunga, Mbeya
HOSPITALI teule ya wilaya ya Mbeya(Ifisi-Mbalizi), imekumbwa na
kashfa ya kufukuza wajawazito wodini kisha wajawazito hao kujifungulia
katika mazingira yasiyo na staha nje ya hospitali.
Tukio la hivi karibuni limetokea usiku wa Desemba 19, mwaka huu,
ambapo baadhi ya wauguzi waliokuwepo katika chumba cha matazamio ya
kujifungua, wanadaiwa kumfukuza na kumpiga mjamzito Sabina Mwakyusa(28)
mkazi wa Kijiji cha Iwala, kata ya Utengule Usongwe wilayani humo.
Akizungumza na kalulunga media blog, Sabina, alisema alifika
hospitalini hapo Desemba 18, mwaka huu na alipimwa na manesi ambapo
walimwambia kuwa hawamuoni mtoto tumboni mwake.
‘’Baadaye akaja Daktari na kunipima, akaniambia mtoto anaonekana
vizuri na ningejifungua mtoto wa kike ndipo nikaendelea kusubiri uchungu
zaidi’’ alisema Sabina.
Alisema ulipofika usiku wa Desemba 19 majira ya saa mbili usiku,
alianza kujisikia uchungu, ndipo manesi waliompima mwanzo wakamwambia
anatakiwa apimwe tena jambo ambalo alikataa kwa madai kuwa alikuwa
akiumizwa, ndipo wakamwambia aondoke hospitalini hapo kwasababu ana
kiburi.
‘’Baada ya kuonekana mimi nasita kuondoka, wakaanza kunipiga na
kunipatia biki na kunilazimisha kuandika kuwa mimi sitaki kujifungulia
hapo ndipo tukatoka na mama na kwenda nje ya geti na kujifungulia getini
huku mvua ikinyesha’’alisema Sabina Mwakyusa.
Alisema, mama yake na baadhi ya wajawazito waliokuwepo ndani ya
wodi hilo, walijaribu kuwabembeleza wasimfukuze lakini walikataa.
Mama mzazi wa mwanamke huyo, Roda Mwakyusa(50), alisema anaumia akikumbuka yaliyomkuta mwanaye ikiwa ni uzao wake wa kwanza.
‘’Niligaragara mweeeh! kuwaomba msamaha wale manesi ili wamsamehe
na kumhurumia huyu mtoto wangu, lakini walikataa wakisema kuwa ana
kiburi sana’’ alisema Prisca Mwakyusa.
Alisema walipotoka wodini huku mwanaye uchungu ukimzidi, walifika
getini akazidiwa. Chupa ikapasuka. Damu zikaanza kumvuja; alikaa muda
mrefu zaidi ya saa moja na kuanza kujifungua ndipo walinzi wa kampuni ya
Mult-Lion, wakamsaidia kumpeleka katika upenu wa duka la hospitali hiyo
ili kukwepa kokoto zilizopo na mvua iliyokuwa ikinyesha.
Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Mult-Lion, Kinanda Sanga,
alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema kuwa hakuwa na taarifa lakini
baada ya kuwauliza askari wake walimpatia taarifa ya tukio hilo kuwa
lilitokea na wao wakatoa msaada.
Dada wa msichana huyo, Enitha Mwakyusa(35), alisema alipigiwa simu
majira ya saa tano usiku na mama yake mzazi akimweleza yaliyomkuta mdogo
wake na kwamba atafute gari la kwenda kuwachukua.
‘’Mama alinipigia simu usiku, nikawaamusha majirani ambao walikuwa
na namba za madereva tax, ambapo saa saba walifika hapa nyumbani
Mapelele’’ alisema Enitha.
Wifi wa Sabina Mwakyusa, Prisca Nafred, alisema alimpeleka mtoto
aliyezaliwa katika hospitali hiyo majira ya saa saba mchana ya Desemba
20, kwa ajili ya chanjo, lakini hakupata chanjo kwa madai kuwa alikuwa
amechelewa kufika, hivyo alitakiwa kufika siku ya Jumanne Desemba 24,
mwaka huu.
Desemba 21, familia hiyo ilimpigia simu Mwandishi wa habari
wakimweleza kuhusu maendeleo mabaya ya mtoto ambapo Mwandishi wa habari
hizi alimtaarifu Mratibu wa afya ya mama na mtoto mkoa wa Mbeya, Prisca
Butuyuyu, kuhusu suala hilo ambapo makubaliano yaliafikiwa kuwa mtoto
apelekwe Hospitali ya Rufaa, kitengo cha wazazi Meta.
Mtoto huyo alipokelewa Meta na kuingizwa kwenye chumba cha joto
kisha kuanza kupatiwa matibabu kwa kuwekewa drip za maji mpaka Desemba
23 mwaka huu.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbeya Louis Chomboko, alipopata taarifa,
alichukua hatua ya kwenda kumuona mtoto huyo katika hospitali ya Meta.
‘’Nimeonana na mama wa mtoto na kumuona mtoto chumba cha joto na
kupata maelezo yote ikiwa ni pamoja na maelezo ya file la Meta hivyo
nipe nafasi tena kufuatilia tukio hili hospitali ya Ifisi na tukibaini
ukweli tutachukua hatua’’ alisema Dr, Chomboko akimsihi Mwandishi
kutoandika kwanza habari hii.
Mganga mkuu wa hospitali ya Ifisi Mbalizi, Msafiri Kimaro, Desemba
23, mwaka huu, alipotakiwa kuzungumza na mwandishi wa habari, aliitisha
kikao cha wauguzi wanne waliokuwepo siku ya tukio, Muuguzi mkuu, muuguzi
kitengo cha chanjo idara ya Mama na mtoto na katibu wa hospitali hiyo.
Alisema katika hospitali hiyo, wanawake zaidi ya 300 wanajifungulia
hapo lakini tukio kama hilo hakumbuki kuwahi kujitokeza ingawa Muuguzi
mkuu alikiri kuwa anayeonekana kukataa kupata huduma hapo anaandika
maelezo na kuruhusiwa kuondoka.
Dr. Kimaro, aliwauliza wauguzi waliokuwepo siku ya tukio, ambapo
walikubali kumfahamu mjamzito huyo na kukubali kuwa alikuwa chini yao na
kwamba alikataa kupata huduma hospitalini hapo na kuamua kuondoka.
‘’Ilipofika saa mbili alipatwa uchungu na tulipotaka kumpima kwa
kumwingiza vidole sehemu za siri alikataa na pia siku ya kwanza
alitusumbua sana na kubana miguu, ndipo akaandika maelezo mafupi kuwa
hakutaka kupimwa bali kwenda yumbani kwake’’ alisema Tumaini Mgimwa.
Aliongeza kuwa mama yake mzazi wa Sabina, alimbembeleza mwanaye ili
akubali lakini alikataa ndipo mama yake akaanza kulia akimtaka akubali
lakini hakuweza kukubali kutibiwa hospitalini hapo.
‘’Muuguzi mkuu wa hospitali hiyo, Sikitu Mbilinyi, alisema yeye
alikuwepo siku hiyo na alipoitwa akakutana na mgonjwa lakini mjamzito
huyo alikataa kutibiwa ndipo akawaambia manesi kuwa mgonjwa asiondoke
mpaka asaini kuwa hataki kutibiwa’’ alisema Mbilinyi.
Alisema mgonjwa kukataa au kukubali kupewa huduma na hospitali au
daktari fulani ni haki yake lakini wengi hawajui haki zao na kwamba
mjamzito huyo alipojifungulia katika geti la hospitali hiyo, mama yake
angepaswa kuingia ndani ambako anadai eti wangempatia msaada.
Katibu wa hospitali hiyo, Goodluck Lession, alisema swali la msingi
ni kwamba iweje mjamzito afike tangu Desemba 18 mpaka usiku wa kuamkia
Desemba 20, kisha aseme kuwa hataki kupata huduma hospitalini hapo?
Goodluck, alisema hayo baada ya swali kutoka kwa mwandishi kumhoji muuguzi mkuu Mbilinyi swali hilo.
Kwa upande wa kiongozi wa kitengo cha chanjo hospitalini hapo,
alisema kuwa kukataliwa chanjo mtoto huyo ni kutokana na dawa ya chanjo
inatakiwa chupa moja kuchanjwa watoto kumi.
‘’Tunafanya hivyo kwasababu endapo mtu ukichanja mtoto mmoja,
inatakiwa dawa hiyo uiandikie maelezo hivyo tunaogopa’’ alisema kiongozi
huyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya kanisa la Uinjilisti Tanzania,
ambalo linamiliki hospitali hiyo na serikali kuingia ubia, Tito Nduka,
alipohojiwa kuhusiana na jambo hilo, alisema kuwa amepata taarifa kuwa
hospitali imeshusha ufanisi wa kazi.
‘’Kwanza kamati kuu yetu imepata taarifa za kudhorota kwa huduma
kwa ujumla, lakini Mganga mkuu ni mwadilifu na msikivu, katika jambo
hilo tutakaa na viongozi na kulikemea’’ Alisema Nduka.
Katibu Mkuu wa maendeleo ya kanisa hilo, JaCkob Mwakasole, alisema
taarifa za kushuka kwa ufanisi wa huduma katika hospitali hiyo
wamezipata na kwamba tukio hilo haliwezi kupita hivi hivi.
Mratibu wa afya ya Mama na mtoto mkoa wa Mbeya, Prisca Butuyuyu, alisema kuwa….
Mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya, ………. Seif Mhina, alisema kuwa…
Baadhi ya wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo ambao hawakutaka
majina yao kuandikwa, wamekiri kuwepo kwa udhorotaji wa huduma za afya
katika hospitali hiyo tangu ubia wa serikali na kanisa na kwamba mpaka
sasa kuna maelewano hasi kati ya waajiriwa wa serikali na wale wa kanisa
jambo ambalo wanaoumia ni wagonjwa.
Wakati hayo yakiedelea kutokea nchini, malengo ya milenia yanaeleza kutaka kupunguza vifo vya mama na mtoto ifikapo mwaka 2015.
Hayo yanabainika katika utafiti wa umoja wa Mataifa, unaongelea
“ndoto” ya kufikia malengo nane ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) zaidi
katika afya: kupunguza vifo vya watoto wachanga (Lengo la 4), kuboresha
afya ya wajawazito (lengo la 5) na kukabiliana na VVU/UKIMWI, malaria na
magonjwa mengine (Lengo 6).
Baadhi ya viongozi wa dunia wanaoongoza mtandao wa kutoa
msukumo wa kisiasa ni pamoja na Rais Michelle Bachelet wa Chile, Rais
wa Msumbiji Armando Guebuza na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Daktari bingwa nchini katika masula ya uzazi, Dr. Moke Mgoma,
kutoka shirika la Evidence for action(E4A), alipohojiwa alisema
alichotendewa Sabina Mwakyusa, ni kitendo kibaya ikizingatiwa kuwa
serikali inafanya jitihada kuondoa ukatili wa baadhi ya wauguzi.
Mwezi Desemba mwaka 2012, Mama mmoja(jina tunalo), aliyekuwa
anaumwa BP, alichomwa sindano (dawa)ambazo haziendani na ugonjwa wake na
mmoja wa watoto wake alipohoji kwa uongozi wa hospitali hiyo alijibiwa
kuwa hapaswi kugombana na wauguzi! Kisha akaitwa Dr. Kenneth, ambaye
aliamua kuokoa maisha ya mama huyo katika hospitali hiyo ya Ifisi kwa
kumchoma sindano ya dawa iliyokuwa ikitakiwa.
–KALULUNGA–