Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, atua Yanga


Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic. Na Mwandishi Wetu KOCHA wa Simba, Zdravko Logarusic sasa ndiyo chaguo la kwanza la Yanga katika nafasi ya kocha mpya iliyoachwa na Ernie Brandts. Taarifa za uhakika zinasema tayari Yanga imetuma mtu afanye mazungumzo na kocha huyo raia wa Croatia ambaye anaonekana atawezana na mastaa wa Jangwani. Mtoa habari ameliambia Championi Jumatano, jana mchana kuwa Yanga wamemtuma mtu huyo kufanya mazungumzo na Logarusic. “Mtu huyo ndiye atazungumza na kocha ili kuangalia kama atakubali kutua Yanga, unajua ana mkataba wa miezi sita tu. Hivyo pamoja na pilika za Yanga kutafuta kocha, lakini inaonekana chaguo namba moja ni huyo wa Simba,” kilieleza chanzo. Juzi, Logarusic alisema anauheshimu mkataba wake wa miezi sita Simba ingawa hakukanusha au kukubali lakini jana simu yake ilikuwa haipokelewi, wala hakuna ujumbe aliojibu pamoja na kuulizwa maswali kadhaa na gazeti hili kama ameishamalizana na Jangwani. Chaguo la pili la Yanga limeelezwa kuwa ni Bobby Williamson anayefundisha Gor Mahia ya Kenya ambaye jana alizungumza na Championi na kusisitiza. “Mara zote nimesema wazungumze na uongozi, mkataba wangu unaisha mwezi wa saba, kama watakuwa tayari kuniachia sawa ila hapa nilipo nina furaha,” alisema. Tayari uongozi wa Gor Mahia umeonyesha hauna tatizo na umeikaribisha Yanga kuzungumza ili kupata mwafaka kuhusiana na kocha huyo raia wa Scotland. Sababu kadhaa zinaonyesha tayari Logarusic ametua Yanga mguu mmoja: Mkataba: Mkataba wake ni wa miezi sita tu na unamruhusu kuondoka bila ya masharti kwa kuwa alikuwa chini ya uangalizi, hivyo inakuwa rahisi zaidi kwa Yanga. Mshahara: Mshahara wake Simba ni dola 3,000 (Sh milioni 4.8 tu), wakati Brandts alikuwa anachota dola 11,000 (Sh milioni 18) katika mkataba wake mpya. Hivyo, ni rahisi kumshawishi kama atapewa angalau hata mara mbili au tatu ya mshahara wake wa sasa Simba na akarukia upande wa pili. Viongozi: Inaonekana viongozi Yanga wameshindwa kujizuia, kuonyesha ‘mapendo’ kwake kutokana na uwezo aliouonyesha wa kuibadilisha Simba ndani ya muda mfupi. Lakini alionyesha hahofii nyota yoyote siku alipoichapa Yanga 3-1, maana alikuwa anabadilisha wachezaji hata kama ni nahodha.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...