Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Uwanja wa Ndege wa
Dar es Salam (JNIA) jana kilimkamata mwanamke mmoja, Salama Omari
Muzara akiwa amemeza kete za dawa za kulevya aina ya Heroin ambazo idadi
yake kamili haijajulikana.
Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa
za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema, msichana huyo alikamatwa jana saa
saba mchana akiwa njiani kuelekea Macao, China na Shirika la Ndege la
Ethiopia.
“Alikuwa anasafiri kwenda Macao, China kwa ndege
ya Ethiopian Airlines ambayo ilikuwa iondoke saa 10 jioni ndipo kikosi
kazi cha polisi uwanja wa ndege kikamshuku kuwa amebeba kitu kisicho cha
kawaida” alisema Nzowa.
Nzowa alisema, mwanamke huyo alikuwa na hati ya
kusafiria namba AB548242 ambayo ilitolewa Oktoba mwaka jana na
haikufahamika idadi kamili ya pipi alizomeza kwani mpaka sasa bado
anazitoa. Nzowa alisema mpaka sasa mwanamke huyo tayari ameshatoa pipi
kadhaa tangu alipokamatwa jana mchana ambapo kuanzia asubuhi leo hadi
saa saba mchana huu ameshatoa pipi 27.
Kamishna Nzowa alisema hiyo ni sehemu tu ya
mapambano ya dawa za kulevya nchini ambayo imesaidia kupunguza kwa kiasi
kikubwa wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo.
Hivi karibuni, Mwanamitindo wa Tanzania, Jackline
Cliff alikamatwa na kete 66 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye
thamani ya dola za Marekani 137,720 huko Macao, China.
Mwanamitindo huyo , aliyekuwa akisafiri kutoka
Thailand akielekea Macao aliwaambia polisi kuwa alikuwa anaelekea
Guangzhou ambao ni mji wa jimbo la Guangdong huko China.
Kamanda Nzowa alisema kikosi chake kinaendelea
kuwasiliana na Polisi wa Macao ili kujua iwapo ataweza kurejeshwa nchini
ingawa alikiri suala hilo limekuwa gumu kwani China hawana utaratibu wa
kubadilishana wafungwa.
Chanzo:Mwananchi