MAHAKAMA YASHIKILIA UANACHAMA WA ZITTO

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, akitoka chumba namba moja cha Mahakama Kuu jana. 
 
Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, jana ilikubali maombi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya kutaka asijadiliwe uanachama wake na Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Kadhalika, imesema maombi ya mbunge huyo yana sababu za msingi na ndiyo sababu mahakama hiyo imeona ana haki ya kusikilizwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana saa 11:50 jioni na Jaji John Utamwa baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kuhusu maombi ya Zitto.

Saa 9:46 mchana ukumbi namba moja wa mahakama hiyo ulikuwa umefurika wanachama wa Chadema, wanasheria na wanahabari pamoja na Zitto aliyekuwa chini ya ulinzi mkali wa mabaunsa wake na makachero.

Mahakama hiyo ilipanga kusoma uamuzi huo saa 8: 00 mchana, lakini kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika, ilianza saa 9 alasiri.

Jaji Utamwa alisema Januari 2, mwaka huu mahakama hiyo ilitoa zuio la muda baada ya Zitto kuwasilisha maombi ya kuitaka Kamati Kuu ya Chadema kutojadili uanachama wake.
Zitto aliwakilishwa na wakili Albert Msando na Chadema kiliwakilishwa na Tundu Lissu na Peter Kibatala.

Jaji alisema upande wa walalamikiwa uliwasilisha pingamizi la awali kupitia hati ya kiapo iliyoapwa na Kibatala.

Hata hivyo, wakili Msando alipinga kwa madai kuwa baadhi ya hoja zilizokuwa kwenye kiapo hicho hazikuwa na ushahidi ni maneno ya kusikia.

Jaji huyo alisema mahakama imeona kiapo hicho hakina mashiko ya kisheria na imekitupilia mbali na maombi ya mlalamikaji yamekubaliwa.

“Pia, Dk. Willibrod Slaa (Katibu Mkuu) hakuwasilisha kiapo kilichounga mkono pingamizi la awali la walalamikiwa,” alisema Jaji Utamwa.

Baada ya kusoma uamuzi huo, mahakama iliyokuwa imetawaliwa na kelele za watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema ilikuwa na hali ya utulivu.
Zitto alitolewa nje ya ukumbi wa mahakama hiyo kupitia mlango wanaotumia majaji akiwa chini ya ulinzi mkali pamoja na wakili wake.

LISSU: ZITO MBUNGE WA MAHAKAMA
Lisu alisema tangu awali alijua kwamba Zitto ni mbunge wa mahakama.
“Mimi nilisema tangu siku ya kwanza Zitto ni mbunge wa mahakama na siyo wa Chadema. Leo mahakama imethibitisha tena kwamba ni mbunge wa tatu wa mahakama wa kwanza ni Hamad Rashid na David Kafulila,” alisema Lissu.

Naye Wakili Kibatala alisema Jaji ametupilia mbali hati ya kiapo kutokana na kuwa na upungufu wa kisheria, hivyo uamuzi wa mahakama uheshimiwe.

MSONDO: UAMUZI UHESHIMIKE
Wakili Msando alisema mahakama imeangalia maombi ya Zitto yana mashiko ya kisheria na kwamba uamuzi huo uheshimiwe.
“Huo ndiyo uamuzi wa mahakama, uheshimiwe… mahakama imejiridhisha na imetoa uamuzi wake,” alisema Msando.

Katika kesi ya msingi, Zitto analalamikia Baraza la Wadhamini la Chadema na Katibu Mkuu, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Zitto pia anaiomba mahakama kuiamuru Kamati Kuu na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Kadhalika, anaiomba imwamuru Katibu Mkuu kumkabidhi nakala za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua nafasi yake ya unaibu Katibu mkuu ili akate rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.

Akiwasilisha hoja zake, wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika chama, uliotolewa katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Novemba 12 mwaka 2013.

Uamuzi huo unamfanya Zitto aendelee kuwa mbunge kwa kuwa Jaji Utamwa angeamua vinginevyo, Zitto angepoteza uanachama kama wenzake Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, ambao mwishoni mwa wiki Kamati Kuu iliwafukuza baada ya Kitila kushindwa kutoa utetezi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikiwakabili za kukisaliti chama kwa kuanda waraka ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa unapanga kuuondoa uongozi wa sasa.

Mwaigamba alitimuliwa baada ya kuondoka katika kikao kabla ya kuhojiwa na bila kutoa taarifa.

Hamad Rashid Mohamed, Mbunge wa Wawi (CUF) alivuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la CUF kwa tuhuma za usaliti, lakini alikwenda mahakamani kuweka zuio na hadi sasa ni Mbunge, lakini chama hicho hakimtambui.

Naye Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) alivuliwa uanachama na chama chake kwa tuhuma za uasi, lakini aliweka zuio mahakamani. Hadi leo ni mbunge na kuna taarifa kuwa kulikuwapo na mpango wa kufikiwa suluhu kati yake na chama.


HALI NJE YA MAHAKAMA
Hali ya ulinzi nje ya mahakama iliimarishwa tangu saa 6:30 mchana kwa polisi kufanya doria wakiwa na magari manne pamoja na gari kubwa la maji ya kuwasha.

MWENYEKITI BAVICHA AJERUHIWA
Ilipofika saa 7: 56 mchana, zilizuka vurugu zilizohusisha wanachama wa Chadema na wafuasi wa Zitto kurushiana mawe nje ya mahakama hiyo na kusababisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa Kata ya Gongolamboto, Theophil Luyoga, kujeruhiwa kichwani.

Baada ya kujeruhiwa kwa Luyoga, polisi waliokuwapo eneo hilo waliingilia kati na kuyatawanya makundi hayo na muda mfupi baadaye kuwatenganisha kwa kuwawekea mipaka.
Muda mfupi baadaye Luyoga, alipakizwa kwenye pikipiki na baadhi ya viongozi wa Chadema na kupelekwa kituo kikuu cha kati cha polisi kwa ajili ya kuandikiwa PF3 na kupelekwa hospitali.

Nyimbo za kukashifiana pamoja na mabango mbalimbali yaliyokuwa yakimwelezea Zitto yalitawala nje ya Mahakama hiyo.

Moja ya bango walilokuwa nalo wanachama wa Chadema lilisomeka 'Zitto unafiki umekuponza' huku wafuasi wake wakiwa na bango lililosomeka 'Zitto kama Mandela'.
Baada ya kutolewa uamuzi wa mahakama, Lissu aliwafuata wanachama wa chama hicho na kuwaeleza yaliyoamuliwa huku wafuasi wa Zitto waliokuwa na ngoma wakishangilia kwa kuimba nyimbo. 
CHANZO: NIPASHE


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...