Bibi kizee, Mwamini Abdallah |
UONEVU! Bibi kizee, Mwamini Abdallah
anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 100 (alikuwepo wakati wa
Vita ya Kwanza ya Dunia ya 1914), anadai kunyang’anywa shamba na ndugu
zake kisha kutelekezwa na kumsababishia kuishi kwa tabu.
Akizungumza
na waandishi wetu, bibi huyo anayeishi katika Kijiji cha
Ngeleka-Usagara mkoani hapa alidai kwamba aliingia kwenye mgogoro wa
mirathi na ndugu zake aliochangia nao baba mara baada ya mzazi wake
huyo kufariki dunia.
Bibi huyo alisema kuwa mgogoro huo
ulisababisha kufunguliwa kwa kesi Mahakama ya Mwanzo ya Misungwi na
hukumu kuwapa haki ndugu zake hao na yeye kuambulia ardhi kidogo.
Hata hivyo, aliiuza ardhi hiyo kidogo aliyopewa baada ya kukosa huduma za msingi mara alipotengwa na ndugu zake.
Waandishi
wetu wamejionea hali ya bibi huyo ambaye analala chini akitandika na
kujifunika magunia huku paa la ‘kibanda’ anachoishi likivuja.
Kikongwe huyo anapata msaada kidogo kutoka kwa jirani yake Halima Said anayemchotea maji na kumpatia akiba kidogo ya chakula.
Alisema kuwa hata kibanda hicho cha
matope anachoishi kwa sasa alijengewa na mama mmoja aliyekuwa nesi
maeneo hayo lakini kwa sasa kipo hatarini kubomolewa kutokana na
kujengwa kwenye hifadhi ya barabara inayotengenezwa kutoka Usagara
kwenda Kisesa.
“Nalelomba bhamunhu mnahmbilije naphandike hakulalaa niishiliwa,”
alisema bibi huyo kwa Lugha ya Kisukuma akimaanisha ‘naombeni mnisaidie sehemu ya kulala na chakula.’
Kufuatia
ugumu wa maisha ya bibi huyo, mjukuu wake, Mariam John (15) ndiye
anayemsaidia kwa kufanya kazi za ndani Mwanza mjini kwa ujira wa Sh.
20,000/= kwa mwezi, fedha ambazo pia hazikidhi mahitaji yao binafsi. Kwa
yeyote atakayeguswa na mateso anayopata bibi huyu na anataka kutoa
msaada wake, awasiliane na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa
asasi ya FARIJIKA kwa namba 0787 040 261 au 075 604 026.