Kama umewahi kujiuliza kwanini ulikuwa husikii nyimbo za Diamond Platnumz kupitia kituo cha Magic FM cha Dar es salaam pamoja na kituo cha TV Channel Ten kwa kipindi kirefu, jibu ni kwamba msanii huyo ambaye nyota yake inazidi kung’ara kila kukicha aliwahi kukikosea kituo hicho, kwa lugha ya mtaani ‘alizingua’.
Diamond akiwa katika studio za Magic FM
Kwa mujibu wa Salmamsangi.com, Jumatano ya wiki hii (Jan 8) kupitia kipindi cha Daladala Beats cha Magic FM, Diamond akiwa Live kwenye kipindi hicho aliomba msamaha na kusema kuwa alikuwa na tofauti na Radio hiyo kutokana na mambo ya kibinadamu.
Diamond ambaye wiki hii ameachia video na audio ya ‘Number 1 RMX’ aliyomshirikisha Davido wa Naija, alifika katika studio za Magic akiwa ameongozana na Meneja wake Babu Tale wa Tip Top Connection pamoja na Said Fella.
Baada ya kuomba msamaha hewani sasa nyimbo za Platnumz zimeanza kupata airtime kupitia vipindi mbalimbali vya Radio hiyo ambayo ilisitisha kupiga kazi zake kwa takribani mwaka mmoja na nusu toka tofauti hizo zilipojitokeza.