WAZIRI
PROF. MAGHEMBE AJIULUZU; DAWASA/DAWASCO WAREJESHE HUDUMA NDANI YA WIKI MOJA
KATIKA MAENEO YALIYOKUWA YAKIPATA MGAWO WA MAJI KABLA
Aidha, Wenyeviti wa
Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini
(DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo
ya maji kujirudia rudia katika Jiji la Dar Es Salaam.
Pia, wajieleze kwa umma
ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais awachukulie kwa uzembe, kuisababishia
hasara Serikali, kuathiri uchumi wa nchi
na maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya msingi
ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.
Itakumbukwa kwamba
tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni juu ya hatua za
haraka za kuboresha upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam,
nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kuchukua hatua za
haraka.
Iwapo hoja hiyo
ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar
Es Salaam mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali
kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.
Hata hivyo, badala ya
kuunga mkono hoja hiyo ambayo ingeisaidia Wizara yake na kurekebisha udhaifu uliokuwepo na hivyo
kumrejeshea imani kwa umma ambavyo ilikuwa imepungua; Waziri Maghembe akaamua
kinyume cha kanuni za Bunge kutoa hoja ya kuondoa hoja niliyowasilisha.
Katika hatua hiyo
nilijaribu kutumia kanuni za Bunge kuweza kutoa ufafanuzi juu ya uongo wa
Waziri Prof. Maghembe na hatua ambazo Bunge lilipaswa kuchukua. Hata hivyo
Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai aliamua kukiuka kanuni kumlinda hali ambayo
ilichochea vurugu bungeni.
Mara baada ya kurejea
bungeni tarehe 10 Februari 2013 nilihutubia wananchi na kuwaeleza kusudio la
kuandaa maaandamano kwenda Wizara ya Maji iwapo katika kipindi cha ndani ya
wiki mbili Waziri Prof. Maghembe asingejitokeza kutoa maelezo kwa umma kuhusu
masuala yote ambayo alipaswa kuyajibu bungeni juu ya hatua za haraka
zilizopaswa kuchukuliwa.
Ndani ya wiki hizo
mbili Waziri Maghembe alijitokeza mara mbili kuzungumzia masuala ya maji Dar Es
Salaam; kupitia mikutano ya CCM ikiwemo katika kata ya Goba jimboni Ubungo na
katika mkutano wake na wafanyakazi DAWASA na DAWASCO tarehe 21 Februari 2013 na
kueleza hatua za haraka ambazo angesimamia zichukuliwe.
Hata hivyo, baada ya
wiki moja bila ya Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla kuonyesha kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA,
DAWASA, DAWASCO na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo
nilizieleza kwenye hoja binafsi, niliamua kuchukua hatua zaidi.
Nilitangaza kuongoza
maandamano ya wananchi tarehe 16 Machi 2013 kwenda Wizara ya Maji ili kupata
majibu na kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka. Hata hivyo maandamano
hayo yalizuiliwa na Jeshi la Polisi kwa sababu zisizo za msingi na kuombwa
kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Nilikata rufaa lakini
toka wakati huo mpaka anaondelewa katika nafasi yake Waziri Dr Emmanuel Nchimbi
alikwepa kuchukua hatua dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kinondoni Charles Kenyela kwa kuvunja sheria, kusababisha hasara na kuwanyima
haki ya msingi wananchi ya kufikisha ujumbe kwa Serikali.
Maandamano hayo
yangefanyika na hatua kuchukuliwa matatizo yangepungua tofauti na ilivyo sasa,
hivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Pereira Silima anapaswa kueleza umma lini
rufaa hiyo itashughulikiwa maandamano yaweze kufanyika wananchi wapate majibu
ya hatua za haraka nilizopendekeza ndani na nje ya Bunge.
Zaidi ya nusu mwaka
umepita toka Waziri Prof. Maghembe atoe ahadi ambazo ameshindwa kusimamia
utekelezaji wake na hivyo kupaswa kujiuzulu. Iwapo Waziri Prof. Maghembe
hatajiuzulu nitaeleza hatua zaidi ambazo nitachukua.
Wakati hatua hizo
zikisubiriwa, natoa mwito kwa DAWASA na DAWASCO kuhakikisha kwamba katika
kipindi kisichozidi wiki moja huduma za maji zinarejea katika maeneo ambayo
yalikuwa yakipata mgawo wa maji.
Wenu katika uwakilishi
wa wananchi,
John
Mnyika (Mb)
10/01/2013Source:
Chadema Blog