Profesa
Emanuel Mjema
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),
tawi la Dar es salaam, kimemfukuza kazi mhadhiri wa chuo hicho anayedaiwa
kuhusika na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwamo kufanya
ngono. Mhadhiri huyo ambaye jina halikutajwa alinaswa na kamera za kisasa
za kurekodi matukio za CCTV zilizofungwa kwenye vyumba vya madarasa ili
kudhibiti nidhamu, miongoni mwa wanafunzi na wahadhiri.Kamera hizo zimefungwa
kwenye vyumba vya madarasa 20 ili kudhibiti vitendo vya ngono baina ya walimu
na wanafunzi, wizi wa mitihani na matendo mengine yanayovunja sheria.
Hayo yalibainishwa jana jijini na mkuu wa chuo hicho, Profesa
Emanuel Mjema (pichani), alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa ziara ya
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene.
Profesa
Mjema, alisema, walifikia maamuzi ya kuweka kamera hizo za kisasa
ndani ya madarasa Aprili mwaka jana baada ya kujiridhisha na taarifa za kuwapo
matukio ya ukosefu wa maadili miongoni mwa wahadhiri ikiwa ni pamoja na kutoa
alama za juu kwa baadhi ya wanafunzi wa kike baada ya vitendo vya
ngono.
“Nilipoingia
chuoni hapa Januari mwaka jana, nilisikia kuwa kuna baadhi ya wahadhiri
wamekosa maadili, wanatoa alama za juu kwa wanafunzi wa kike kwa masharti hata
kama hawajafaulu kwa kiwango hicho. Nikaona vyema tuweke vifaa hivyo ili
kudhibiti vitendo hivyo,” alifafanua Profesa Mjema.
Alieleza kuwa baada ya kuweka kamera hizo 20 kwa kila darasa
kuwa na kamera moja, walifanikiwa kumnasa mwalimu mmoja kwa kitendo cha kukiuka
maadili yake ya kazi na kumfukuza kazi.
Alisema kuwa, kamera hizo pia, zinasaidia kuwadhibiti
wanafunzi wenye tabia ya kuiba mitihani, kwani mikakati iliyopo hata wakufunzi
na wanafunzi hawajui anayetunga mitihani ili mradi ipo ndani ya silabasi ya
chuo.
Kamera hizo zinadaiwa kuwa na uwezo wa kumvuta karibu
mwanafunzi aliyeko darasani na kujua anachokiandika, pia mhadhiri iwapo
anachokifundisha ni cha ukweli au anadanganya kwa hiyo zinatumiwa wakati wote
kwenye vipindi na mitihani.
Alisema, chuo kimeajiri walinzi kwa ajili ya kuwadhibiti
wanafunzi ambao wanavaa nguo ambazo hazina maadili mazuri na pia hukagua
vitambulisho wanapofika getini, lengo likiwa ni kukifanya chuo hicho kubakia
katika heshima yake.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri, Mbene, alipongeza jitihada hizo zilizofanywa na chuo
hicho, huku akikemea vikali tabia inayofanywa na baadhi ya wahadhiri hao,
akiongeza kuwa, ni lazima mwanafunzi apewe madaraja ya matokeo ya mitihani
kutokana na ufaulu na uwezo wake.
Pia,
aliahidi kushughulikia suala la uvamizi wa eneo la chuo hicho pamoja na maombi
ya kuongezewa madarasa ikiwa ni pamoja na kupewa majengo ya Wakala wa Hifadhi
ya Chakula cha Taifa (NFRA).
-NIPASHE