Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu amefanya mabadiliko ya
baadhi ya makamanda wa mikoa, wakuu wa upelelezi wa mikoa, wakuu wa
usalama barabarani wa mikoa pamoja na watendaji wengine wa vikosi na
vitengo mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi. Miongoni mwa makamanda wa
mikoa waliofanyiwa mabadiliko ni pamoja na aliyekuwa kamanda wa Mkoa wa
Ruvuma Kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Deusdedit Nsimeki
anayekwenda kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Aliyekuwa kamanda
wa Polisi Mkoa wa Manyara kamishna msaidizi (ACP) Akili Mpwapwa
anakwenda kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. Wengine ni aliyekuwa
Afisa Mnadhimu mkoa wa Lindi Kamishna msaidizi (ACP) Renatha Mzinga
anakuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Lindi, aliyekuwa afisa Mnadhimu Mkoa
wa Dodoma Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Suzan Kaganda amehamishwa
kwenda kuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora na aliyekuwa kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tabora kamishna msaidizi (ACP) Peter Ouma amehamishiwa
Makao Makuu ya Polisi. Zaidi ya hao wengine waliyohamishwa ni pamoja na
aliyekuwa Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mtwara Kamishna msaidizi wa Polisi
(ACP) Eliyakimu Masenga anakwenda kuwa Mkuu wa upelelezi kikosi cha
Tazara, aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Tabora Kamishna msaidizi wa
Polisi (ACP) David Mnyambuga anakwenda kuwa mkuu wa upelelezi mkoa wa
Ilala, na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala, Kamishna msaidizi
wa Polisi (ACP) Juma Bwire, anakwenda kuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa
Tabora . Aidha, aliyekuwa afisa Mnadhimu mkoa wa Tabora Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi (SSP) John Kauga anakuwa mkuu wa upelelezi mkoa wa
Tabora, aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Rombo (SSP) Mrakibu
mwandamizi Ralph Meela anakwenda kuwa mkuu wa upelelezi mkoa wa Mtwara
na aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wa kikosi cha Tazara Mrakibu wa Polisi
(SP) Isack Msengi anakwenda kuwa Kaimu mkuu wa upelelezi mkoa wa Pwani.
Kwa upande wa wakuu wa Polisi wa mikoa wa Usalama Barabarani ni pamoja
na aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Kinondoni, Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi (SSP) Ibrahim Mwamakula ambaye amehamishiwa Trafiki Kanda Maalum
Dar es Salaam, aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Mtwara, Mrakibu
wa Polisi (SP) Awadh Haji anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa
Kinondoni, na Mrakibu wa Polisi (SP) Ezekiel Kiko Mgeni aliyekuwa ofisi
ya RPC Temeke, anakuwa Mkuu wa Trafiki mkoa wa Temeke. Wengine ni
aliyekuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Lindi Mrakibu wa Polisi (SP) James
Kiteleki anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Njombe, aliyekuwa Mkuu
wa Trafiki Mkoa wa Ilala, Mrakibu wa Polisi (SP) Meloe Buzema anakwenda
kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Lindi, aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Trafiki
Mkoa wa Temeke Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Prackson Kibogoyo
anakwenda kuwa Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Pwani, na aliyekuwa Mkuu wa
Trafiki Mkoa wa Njombe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Chacha Nsaho
Maro anakwenda kuwa Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Ilala. Mabadiliko hayo ni
ya kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya Jeshi la
Polisi katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma
bora ya usalama.
Imetolewa na:
Advera Senso-SSP Msemaji wa Jeshi la
Polisi