WAWILI WAONDOLEWA BUNGE LA KATIBA

Dodoma. Uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, umekumbwa na dosari baada ya wajumbe wawili wenye majina na ubini unaofanana, Amina Mweta, kutinga bungeni kila mmoja akidai kuwa mjumbe halali.

Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zinasema wajumbe hao wanaotokea kundi la wafanyakazi, wamelipwa posho za awali lakini walizuiwa kuendelea na taratibu nyingine kusubiri hatima ya utata wa suala lao.
Habari zilisema baada ya kuwasili bungeni, wajumbe hao walijisajili kwa nyakati tofauti na kila mmoja kupewa vitambulisho.Mmoja alipata chenye namba 602 na mwingine 1308.

Wajumbe hao walikiri kulipwa posho ya kujikimu ya Sh80,000 kwa siku kwa muda wa siku 13 unaomalizika Februari 28 mwaka huu ikiwa na maana kwamba kila mmoja alilipwa Sh1,040,000.
Habari zilidai kuwa Amina Mweta wa kwanza anatoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) na mwingine anatoka katika Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU).
Mkanganyiko huo ulitokana na kuwapo kwa sehemu nyingi za usajili wa wajumbe hao kiasi kwamba watumishi wa Bunge walishindwa kubaini kuwapo kwa Amina Mweta wawili kutoka kundi moja.
Mmoja wa kina mama hao anatokea wilayani Mwanga, Kilimanjaro na mwingine Songea, mkoani Ruvuma.
Mweta kutoka Mwanga alisema alipigiwa simu na Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba na kupongezwa kwa kuteuliwa na Rais kuwa mjumbe.
“Mimi ni personal secretary (katibu muhtasi) wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na nilipigiwa simu na Ofisi ya Bunge wiki iliyopita nikipongezwa kwa uteuzi huo,” alisema.
Alisema alipofika na kujisajili baada ya kutoa kitambulisho chenye jina lake, alipewa kitambulisho na kisha kupewa malipo yake ya posho. Mweta kutoka Songea alisema alipigiwa simu na Katibu Mkuu wa COTWU kwamba ameteuliwa na Rais kuwa mjumbe na kutakiwa kuripoti bungeni.
Kama ilivyokuwa kwa mwenzake wa kutoka Mwanga, alisema naye alijisajili na kulipwa posho ya siku 13 na jana alishangaa kukuta mjumbe mwingine mwenye jina kama lake.
Alisema viongozi wa COTWU wamemwambia asubiri wakati wakitafuta usahihi wa nani hasa kati yao mwenye uhalali wa kuwapo bungeni.

Ofisi ya Rais yatoa msimamo
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa kuhusu mkanganyiko huo, alisema hajapata taarifa rasmi lakini watakapozipata watathibitisha nani aliyeteuliwa na Rais kuwa mjumbe wa bunge hilo.
“Aliyeteuliwa na Rais ni mtu mmoja na ndiyo maana huwa tunapenda watu watumie majina matatu kwa sababu kwenye nchini kunaweza kuwa hata na watu 10 wote wanatumia jina moja.
Tukipata taarifa rasmi tutakachofanya ni kuthibitisha nani haswa aliyeteuliwa na Rais ambaye ataendelea kuwa mjumbe na huyo mwingine basi itakuwa ni bahati mbaya,” alisema Balozi Sefue.
 
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa kuhusu utata huo alisema mjumbe halali ni yule aliyetoka Songea.
Hata hivyo, alisema kinachowashangaza ni kwama yule mwenzake wa Mwanga alipotakiwa kurudisha fedha alizopewa kimakosa alisema ameshatumia sehemu kubwa na kubakiza Sh50,000 tu.
MWANANCHI


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...