Naibu Katibu wa Fedha, Mwigulu Nchemba jana katika Bunge
Maalum La Katiba alichafua hali ya hewa baada ya kumwambia Mwenyekiti wa
Chadema Taifa, Freeman Mbowe na mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa
kwamba wanataka wabunge wa bunge hilo watumie kura ya siri badala ya
wazi kwa kuwa ni mashoga.
"Wanaotetea kura ya siri itumike katika kupitisha Katiba ya
Watanzania, wanaunga mkono sera za ushoga, ni wale ambao vyama vyao
vinazaminiwa na wanaotetea sera za ushioga," alisema Nchemba bungeni.
Kutokana na Kauli ya Nchemba, bunge hilo lilipuka likitaka aombe
radhi huku akionyesha kusita kuomba radhi, lakini Makamu Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu Hassan alimtaka aombe radhi mara
kadhaa.
"Mheshimiwa Mwigulu, naomba usimame na kuomba radhi wabunge wenzako, tafadhali simama," alisema Samia
Baada ya kauli ya Makamu Mwenyekiti Samia, Mwigulu alisimama na kusema: "Mheshimwa Makamu Mwenyekiti, Naomba radhi kwa wote
wanaodhani wao wako hivyo kama nilivyosema."
Kauli hiyo ilionekana kuendelea kuwachefua wabunge wa bunge hilo huku
wakimzomea na kumtaka aombe radhi kwa kuwa bado alikuwa hajaomba radhi
moja kwa moja bali kauli yake ilionekana kuwa na utata.
Kwa mara nyingine, Makamu Mwenyekiti, Samia alisimama tena na kumtaka
aombe radhi. "Mheshimiwa Mwigulu tafadhali omba radhi bila condition,
tafadhali, bila kuomba radhi, Bunge haliwezi kuendela, na ninyi wabunge
wengine kaeni kimya bila utulivu hatuwezi kusikilizana, tafadhali,"
alisema Samia.
Baada ya kauli kauli ya Makamu Mwenyekiti, Samia, Mwigulu alisimama
tena na kuomba radhi kwa heshima na bunge kuendelea na utaratibu wake.
"Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, nakiheshimu hicho kiti hapo mbele,
siwezi kudharau, Naomba radhi kwa wote nilowaudhi," alisema Mwigukulu na
kukaa chini.
Baada ya kauli ya Mwigulu ya kuomba radhi, shughuli za bunge ziliendelea kama kawaida.