RAIA
watatu wa Nigeria na mwanamke wa Kitanzania wamekamatwa na polisi
jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kujaribu kusafirisha madawa ya
kulevya kwenda nchini Liberia. Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa walikuwa
mbioni kutuma mihadarahi hiyo, ikiwa kwenye vitabu, kwa kutumia Wakala
wa Usafirishaji Mizigo ya DHL.
Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalumu Dar es Salam, Suleiman Kova alitaja majina ya
Wanaijeria hao kuwa ni Sunday Chaidikaobi (42), Chukwuma Favour (31), na
Franklin Indubuisi (41). Mtanzania aliyebambwa pamoja na Wanaijeria hao
ametajwa kuwa ni bi Hadija Ngoma (43), mkazi wa Kimara Temboni, Dar es
Salaam.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kova, polisi walipata taarifa juzi, Machi 18, kuwa
kuna watu wanne wanajihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya
waliokuwa katika ofisi za DHL zilizopo Barabara ya Sam Nujoma.
Kufuatia
taarifa hizo, Kamanda Kova amesema “makachero walifuatilia suala hilo
na hatimaye siku hiyo saa 8:30 mchana watu hao walikamatwa wakiwa na
kifurushi wakijiandaa kukisafirisha kwenda nchini Liberia.”
Alisema
polisi walipopekua kifurushi hicho, walikuta vitabu vitatu vya
Kiingereza. Walipopekua vitabu hivyo, walikuta madawa aina ya heroin
katika kurasa za mwanzo.
“Katika
vile vitabu kurasa ya kwanza inayofunika lile jalada gumu kwa ndani,
walikuwa wamefunua na kuweka unga huo na katika ukurasa wa nyuma vivyo
hivyo kwa vitabu vyote,”aliongeza.
Unga
huo unaokadiriwa kuwa na uzito wa nusu kilo, umepelekwa kwa mkemia mkuu
wa serikali kwa uchunguzi zaidi kubaini thamani na uthibitisho wa
madawa hayo. H/T HabariLeo
Inaonekana
Wanigeria wanakuja kwa kasi kwenye biashara hii ndani ya Afrika
Mashariki. Miezi kadhaa iliyopita, Wanigeria wawili walikamatwa katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya, wakijaribu
kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya takriban
shilingi milioni 120; kama inavyoonesha video hii hapa chini