PAPAA MSOFFE NA WENZAKE WATAKIWA KUMWANDIKIA DPP BARUA KUHUSU JALADA LAO KUCHELEWESHWA

Papaa Msoffe akiwa kwenye gari la polisi.
Mfanyabiashara maarufu Abubakar Marijan (50) 'Papaa Msoffe' na mwenzake Makongoro Nyerere wanaokabiliwa na kesi ya mauaji, wameshauriwa kuandika barua ya malalamiko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kujua kwa nini jalada la kesi yao linacheleweshwa.

Wakili wa Serikali, Leonard Challo alitoa ushauri huo jana mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa baada ya washitakiwa kuhoji kwanini jalada la kesi linacheleweshwa.

Awali, Wakili Challo aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika na jalada lipo kwa DPP kusubiri maelekezo.

Makongoro alidai wanateseka na kama wamewekwa gerezani kisiasa. 

Challo aliwashauri waandike barua kwa DPP ili wajue kwanini  jalada la kesi yao linachelewa.

Hakimu Riwa aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Washitakiwa wanatuhumiwa Oktoba 11, mwaka 2011 katika eneo la Magomeni Mapipa  jijini Dar es Salaam kwa makusudi walimuua Onesphory Kituli.

Hawakujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu na wataendelea kusota rumande kwa kuwa mashitaka yao hayana dhamana.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...