Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura.
Baadhi
ya watu wanaoendesha shughuli zao katika eneo la Kituo Kikuu cha
Mabasi Ubungo (UBT), wamesema hawakushuhudia kuvamiwa kwa ofisa yeyote
wa benki katika eneo hilo kama ilivyodaiwa na Jeshi la Polisi Kinondoni.
Madai hayo yanafuatia kifo cha dereva wa bajaj, Saleh Said (19) maarufu kama Kibange Moto, aliyefariki dunia Machi 23, mwaka huu kwa kile kinachodaiwa kifo chake hicho kilisababishwa na kupigwa, kujeruhiwa na askari wa Kituo cha Polisi UBT.
Wananchi hao wamesema wameshangazwa na taarifa za jeshi hilo kwamba dereva huyo, alijaribu kuwatoroka askari baada ya kukamatwa kwa msaada wao (wananchi) na kumrudisha kituoni.
Walisema taarifa hizo hazina ukweli wowote, bali polisi wanatafuta njia ya kubadilisha kesi.
Madai hayo yanafuatia kifo cha dereva wa bajaj, Saleh Said (19) maarufu kama Kibange Moto, aliyefariki dunia Machi 23, mwaka huu kwa kile kinachodaiwa kifo chake hicho kilisababishwa na kupigwa, kujeruhiwa na askari wa Kituo cha Polisi UBT.
Wananchi hao wamesema wameshangazwa na taarifa za jeshi hilo kwamba dereva huyo, alijaribu kuwatoroka askari baada ya kukamatwa kwa msaada wao (wananchi) na kumrudisha kituoni.
Walisema taarifa hizo hazina ukweli wowote, bali polisi wanatafuta njia ya kubadilisha kesi.
Kwa mujibu wa wananchi hao, baada ya Saleh kukamatwa, hakukimbia isipokuwa yeye na baadhi ya madereva wenzake, walikwenda kituoni.
Hata hivyo, walisema alipotakiwa kuingizwa mahabusu, Saleh alikataa akidai mpaka afahamu kosa lake.
Walisema baada ya kijana huyo kukataa kuingia mahabusu, mmoja wa askari (jina limehifadhiwa), alianza kumpiga huku baadhi ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo, wakichungulia dirishani.
“Tumeshangaa sana eti polisi wamejieleza kwenye vyombo vya habari kwamba yule dogo (Saleh) aliyekufa juzi kwa kupigwa na askari, alimvamia ofisa mmoja wa benki ya ABC na kumpora fedha na kwamba alipokamatwa alitaka kukimbia lakini alikamatwa na wananchi," alisema mmoja wa wananchi hao kwa sharti la kutotajwa jina lake.
“Hakuna askari wa benki aliyevamiwa na kuporwa hapa Ubungo, na isitoshe hata yule dogo mwenyewe siyo mwizi, ila polisi wanataka tu kumbambika kesi ambayo haipo," aliongeza.
“Alimpiga sana kwa rungu na kumkanyaga sehemu mbalimbali za mwili...baadhi ya watu walipiga kelele ‘unaua!’, lakini yule polisi alijibu kuwa `haiwahusu na hata kama ni kesi tutajibu sisi siyo nyie'" aliongeza.
NIPASHE ilizungumza na wananchi mbalimbali katika eneo hilo la Ubungo ambao kila mtu kwa nyakati tofauti walikana kushiriki kumpiga Saleh wala kushiriki kumkamata bali muda mfupi baada ya kuingizwa kituoni hapo alianza kupigwa na askari.
Pia, baadhi ya wananchi katika kituo hicho waliliambia gazeti hili kwamba tangu wiki iliyopita, hawajawaona kituoni hapo askari polisi waliohusika na tukio hilo.
Hata hivyo, uchunguzi wa NIPASHE wiki iliyopita ulibaini kuwa Saleh alipelekwa katika hospitali ya Sinza Palestina Machi 23, mwaka huu usiku kutibiwa huku kitabu kikionyesha kuwa alipata ajali.
Aidha, taarifa zaidi zilidai kuwa baada ya kijana huyo kutibiwa, alirudishwa Kituo cha Polisi UBT lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na hivyo kurudishwa tena katika hospitali hiyo.
Kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya, Saleh alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala ambako jina lake la Kibange Moto, lilionekana katika daftari la chumba cha kuhifadhia maiti huku sababu za kifo chake zikielezwa kuwa zilitokana na kipigo.
NIPASHE jana lilipiga simu katika matawi yote ya benki ya ABC kumtafuta ofisa wake aliyedaiwa kuporwa na madereva bajaj UBT Machi 23, mwaka huu, lakini lilielezwa kwamba hawamfahamu ofisa huyo.
Babu wa marehemu (Saleh), Deus Martin, alisema matokeo ya awali ya uchunguzi ambayo yalitolewa Machi 27, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, yalionyesha kuwa kijana huyo alipigwa na kuvunjika mshipa wa shingo, damu ilivujia katika mkono na mapafu yalijaa maji.
Pia alisema baada ya matokeo hayo waliamua kumzika marehemu katika makaburi ya Kisutu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, alisema wamemaliza uchunguzi wao lakini utatolewa kwa pamoja na uchunguzi wa daktari.
Saleh alifariki dunia Machi 23, mwaka huu saa 7:00 usiku, huku chanzo cha kifo chake kikionekana kuwa na utata baada ya kuwapo kwa taarifa zinazokinzana kati ya Jeshi la Polisi Kinondoni na wananchi.
CHANZO: NIPASHE