MWANAFUNZI
wa kidato cha nne nchini Burundi, Miburo Anne Mony (17), raia wa nchi
hiyo amesema anakwenda kufia kwao baada ya madaktari ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili kumwambia ugonjwa wake wa kansa umecheleweshwa hivyo si
rahisi kutibika.
HAJUI ATARUDIJE NYUMBANI
Akizungumza
na mwandishi wetu huku akibubujikwa machozi ndani ya Wodi Na. 24, Sewa
Haji, Muhimbili, mwanafunzi huyo wa kike ambaye hajui Kiswahili wala
Kingereza vizuri alisema hajui atarudije kwao Burundi kwa kuwa hana
fedha baada ya kuishiwa.
Aliongeza kwamba alikuwa na matarajio kuwa angepata matibabu hapa Tanzania baada ya huko kwao kushindikana.
UGONJWA ULIVYOANZA
“Ugonjwa huu
ulianza kama uvimbe nikiwa kidato cha kwanza, ulikuwa ikiwasha kupita
kiasi, ulizidi kuvimba kwa kasi ya ajabu, nikakatisha masomo kwa vile
nilianza kupata maumivu makali mno.
“Mama alianza kuhangaika kwa kunipeleka katika hospitali mbalimbali kule kwetu Burundi bila mafanikio.
“Mama
yangu ni mkulima, hana uwezo, alikuwa akitafuta pesa kwa shida kwa vile
baba alishafariki dunia, kwa hiyo majukumu yamekuwa ya kwake. Mama
hakuchoka, alinipeleka Hospitali Kuu ya Roi Khared ambako pia matibabu
yakashindikana, nikarudishwa nyumbani.”
UWEZO WA MAMA UMEKWISHA
“Nilikuwa
natokwa machozi pale nilipowaona wanafunzi wenzangu tuliofaulu nao
wakienda shule huku mimi nikiwa nyumbani na sijui hatima yangu.
Mama naye alivunjika moyo akawa hana pa kunipeleka kwani uwezo wake wa kuzunguka na mimi kifedha ulikwisha. Nilisubiri kifo tu.
“Siku moja
mama aliambiwa na watu kwamba ugonjwa wangu unatibika katika Hospitali
ya Muhimbili hapa Tanzania. Alijiuliza namna ya kunileta huku kwani
nauli na fedha za matumizi alikuwa hana.”
MICHANGO ILICHANGWA
“Nilichangiwa
michango lengo likiwa niletwe Muhimbili, fedha kidogo ilipatikana
likaibuka swali la nani atanileta? Maana mama hajui Kiswahili wala
Kingereza.
Akamuomba
kaka yangu anaitwa Albert ambaye ni mtoto wa baba mkubwa, yeye anafanya
kazi ya kufagia barabara na aliomba ruhusa ya wiki mbili ambayo
inaelekea kwisha sasa.
“Tulipofika
hapa Muhimbili nashukuru tulipokelewa vizuri, nikapata matumaini ya
kipona. Madaktari walinikata nyama ya midomo kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi.”
UGONJWA HAUTIBIKI
“Baadaye
madaktari walinishtua sana, waliniambia eti nina kansa na haiwezi
kutibika maana imekaa kwa muda mrefu. Kwa hiyo sasa natakiwa nirudi
nyumbani hadi hapo Mungu atakapochukua roho yangu.
“Niliposikia
hivyo nilipoteza fahamu, nikazinduka baadaye. Kilichonifanya nizimie ni
kule kuambiwa tegemeo la kupata matibabu hakuna.
“Sina mahalI
pa kwenda tena bali ni kurudi Burundi nikafie kule. Yote namwachia
Mungu, hamna jinsi, nakufa nikijiona,” alimaliza kusema mwanafunzi huyo
huku akibubujikwa machozi.
Kwa upande wake kaka yake Albert alisema wamezunguka kila hospitali kutafuta matibabu bila mafanikio.
“Kwa
sasa nimeishiwa nauli, hatujui tutaendaje nyumbani, nilikwenda kwenye
ubalozi wetu kuomba msaada wakaniambia si rahisi kusaidiwa kwa vile
hatukuletwa na serikali. Sijui nitarudi vipi na huyu mgonjwa,” alisema
Albert.
Anayetaka
kusaidia nauli ya kurudi kwao Burundi anaweza kumchangia kwa
kuwasiliana na Idara ya Ustawi wa Jamii Muhimbili kwa simu namba 0766
534498.