Bunge
limesisitiza kuwa jengo la ghorofa 16 lililoko katika Mtaa wa Indira
Gandhi, Dar es Salaam ambalo liliagiza mwaka jana livunjwe, agizo hilo
litekelezwe.
Aidha, imeishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine.
Mbunge wa
Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) akisoma taarifa hiyo bungeni jana,
alisema, “suala hili tuliliagiza katika bajeti iliyopita na tunazidi
kusisitiza utekelezaji huu ufanyike mara moja.”
“Kamati
inasikitikishwa kwamba agizo hili halijatekelezwa. Kamati inaiagiza
Serikali kulifikisha suala hili kwa Rais haraka ili lipatiwe ufumbuzi
kabla ya madhara kutokea,” alisema Bulaya.
Kuhusu
ardhi, ilishauri Serikali kuondoa mianya inayotoa fursa na ushawishi
mbovu kwa viongozi na watu wachache wasio na nia njema kwa maslahi ya
Taifa, bali kujilimbikizia mali kwa maana ya Taifa kwa kutumia mgongo wa
Serikali.
“Aidha,
Kamati inaishauri Serikali kutaifisha maeneo yote makubwa
yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wananchi kwa matumizi mengine,” alisema
Bulaya.
Kuhusu
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kamati iliishauri Serikali kupitia
Wizara ya Fedha ione umuhimu wa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) kwa nyumba zinazojengwa na shirika kwa ajili ya kuuza kwa wananchi
wa kipato cha chini na kati.
Pia,
ilisema licha ya Serikali kuondoa VAT na ushuru wa Forodha kwa shirika
NHC kwa vifaa vya ujenzi inavyoagiza nje, inaishauri kuliondolea pia
shirika hilo VAT kwa vifaa vya ujenzi vinavyozalishwa nchini.
Aidha,
imeitaka Serikali kulipa deni lililobaki la Sh 4,226,957,203.65 kwa NHC
kutokana na madeni ya Wizara, Taasisi na Idara za Serikali.