Askari polisi mmoja wa kituo cha polisi Chang'ombe, Mkoa wa kipolisi wa Temeke, ameuawa kikatili siku ya ijumaa mchana baada ya kupigwa risasi ya kifua na majambazi waliokuwa wanajaribu kutoroka baada ya kufanya tukio la kihalifu. Askari hao waliokuwa doria katika eneo la Wailes walijikuta wakishambuliwa kwa risasi na majambazi hao mara baada ya majambazi hao kujaribu kukimbia katika eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki kipindi ambapo askari polisi walikuwa karibu na eneo la tukio. Hata hivyo wakati askari hao wakijaribu kuwafukuza majambazi hao wawili kwa lengo la kuwakamata ndipo jambazi mmoja alitoa bastola na kumpiga risasi ya kifua askari huyo na kufariki pale pale.
Hata hivyo katika harakati za kujaribu kukimbia majambazi hao walianguka na pikipiki waliyokuwa wakitumia ndipo wakaamua kutimua mbio mitaani na kuingia katika nyumba moja ambapo walijificha na kujifanya kama ni wakazi wa eneo hilo, baada ya wnanchi na polisi kufika katika nyumba hiyo, baadhi ya majirani waliwaambia polisi kwamba wameona watu hao wameingia katika nyumba hiyo. Baada ya polisi kuingia waliwakuta watu hao wakiwa wametulia kama kwamba wao ni wakaazi wa nyumba hiyo na wala hawajui lililotokea.
Baada ya kuwatambua watu hao, polisi waliwatia nguvuni huku wananchi wenye ghadhabu waking'ang'ania kuwa wanataka kuwaua sababu wameshaua askari mmoja. Baada ya vuta nikuvute kati ya wananchi na askari hao ambao walikuwa wachache, wananchi walifanikiwa kuwachukua majambazi hao kwa nguvu kutoka mikononi mwa polisi na kuanza kuwapiga kwa silaha mbalimbali za kienyeji yakiwemo mawe na marungu mpaka watuhumiwa hao wakapoteza maisha.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo waliiambia blogu hii kwamba majambazi hayo kabla ya kupambana na polisi walikuwa wamefanya uvamizi na kumuibia mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo. Hata hivyo mali au fedha iliyoibiwa haikuweza kujulikana mara moja.