Wasambazaji wa
filamu wanasema hakuna mauzo tena ya filamu toka kifo cha marehemu
Steven Kanumba, wanalalamika kuwa mauzo yameshuka sana hadi hata wengine
kuachana na biashara hiyo na kuamua kufanya biashara nyingine
zinazowalipa.
Inawezekana maneno yao yakawa sahihi au si sahihi,
kutokana na hali halisi ya mfumo wa tasnia ya filamu ulivyo hasa katika
idara ya mauzo, sasa kila mtu anajaribu kutafuta sehemu gani ya
kuangukia ndio tunasikia wakisema kuwa toka kifo cha Kanumba hakuna
mauzo ya filamu.
Ni kweli hakuna
ubishi kuwa Kanumba alikuwa na mvuto wa kipekee katika tasnia ya filamu
Bongo lakini hatuna mbadala wake? Ambaye anaweza kuvaa viatu vyake na
kuifanya tasnia ya filamu ifanye vizuri kama awali! Inashangaza sana
kwani inaonekana kuwa msanii huyo alitengenezwa na kuwa alivyokuwa.
Hivi karibuni
ilitoka tathamini kuwa kuwa filamu zinazoongoza kwa mauzo kwa muda mrefu
ni tano tu, ambazo ni 1. Furaha iko wapo 20%, 2. Kigodoro, 3. Mwali wa
Kizaramo, 4.Bado Natafuta, 5. Ndoa yangu ambayo ni kazi ya marehemu
Kanumba na huku kazi za msanii ambaye hayupo Duniani zikiendelea kufanya
vizuri sokoni.
Ukimtoa Kanumba
hapo utagundua filamu ambazo zinaonekana kufanya vizuri si zilizochezwa
na wale wasanii nyota ambao ndio wamezoeleka kuwa ni vinara vya
kuzalisha filamu Swahiliwood, bali ni kazi zilizofanywa na wasanii
chipukizi au wasiopewa nafasi katika tasnia ya filamu Bongo.
Hivyo
inawezekana ikawa tatizo si kutoweka kwa Kanumba ndio sababu ya kushuka
kwa soko la filamu Swahiliwood, nafikiri una kitu cha kujifunza hapa kwa
wasambazaji wa filamu zetu badala ya kuuza au kusambaza sinema kwa
mazoea wabadilishe mfumo wa usambazaji.
Pengine
ushindani wa wasanii wawili yaani marehemu Kanumba na Ray vilichochea
mbio za tasnia ya filamu na wao kutumika kuwa ni vinara wa tasnia hiyo,
kwani hadi sasa toka kifo cha Kanumba hata muonekano wa Ray umepotea
kabisa haonekani.
Kwa sasa
unaweza kumsikia Ray akiongelewa kuhusu mahusiano yake na msanii
mwenzake Ray na si kuhusu kazi zake anazotengeneza tofauti na hapo
awali, ambapo wasanii watambulika kwa kazi zao, lakini kwa sasa wasanii
wetu wanabainishwa kwa kashifa zinazowakabili kama watu nyota si kwa
kazi zao.
Lakini kuna
tatizo lingine ambalo linaikumba tasnia yetu ya filamu Bongo ni ile hali
ya baadhi ya wasanii kukosa ubunifu na kutafuta mbinu au ubunifu ambao
utawatambulisha wao zaidi ya kutumia muda mwingine kuweka nywele zao
wave ili wafanane na marehemu Kanumba na si kutafuta siri ya mafanikio
yake.
Kuna vitu vingi
ambavyo marehemu aliweza kuvifanya na vikamtambulisha yeye kama ni moja
kati ya wasanii maarufu Tanzania kutokea katika tasnia ya filamu Bongo,
lakini leo hii tunampataje mtu kama yeye jibu ni hakuna, tofauti yake
na waliobaki ni kwamba wameridhika na umaarufu wa ndani si kutafuta njia
za kimataifa.
Tumeona juhudi
za baadhi ya wasanii wa filamu ambao wameweza kujaribu kufuata nyayo
zake kwa mbali sana, mfano ni kama Jacob Stephen ‘JB’ ambaye ameweza
kuingia mikataba na baadhi ya makampuni kama vile Airtel na Steps Solar
pia akiwa mrithi wa nafasi ya marehemu Kanumba kama Balozi wa Oxfarm.
Lakini kuna
kitu kimekosekana kwa JB pamoja na kuwa ni balozi wa makapuni kadhaa
lakini bado hakuna muonekano mkubwa kwake na kuweza kusikika kama
Kanumba hatujui sababu ni nini? Kwani yale yaliyofanywa na Kanumba ndio
ambayo anayafanya JB.
Jb amekuwa
akilaumiwa kwa tabia yake ya kujisikia na kushindwa kutoa ushirikiano
kwa baadhi ya waandishi wa habari pale wanapotaka kuongea naye zaidi ya
wale anaoamini ni rafiki zake ambao anaweza kuwatumia kwa matangazo na
kumsifia sana bila kumkosoa hata kama atakuwa amekosea kama mwanajamii.
Hivyo
tunategemea kuendelea kuliona pengo hilo ambalo ni wazi limeonekana kwa
kupitia kwa wauzaji wa filamu ambao ni wadau wakubwa katika tasnia ya
filamu Swahiliwood, tunahitaji mabadiliko makubwa hasa kwa upande wa
mauzo kwani soko ni baya sana kwa sasa na hakuna juhudi za makusudi
katika kunasuka.
Wasanii na
wadau wa tasnia ya filamu tuna kazi kubwa sana katika kuliweka sawa hili
suala la maslahi ni tatizo kubwa kama halitashughulikiwa tutakuwa
mashuhuda tasnia hiyo ikipotea kama vile muziki wa Bongofleva, lakini
angalau wao wanaweza kupata matamasha na kulipwa hata wasipouza Dvd.
Suala linakuja
kwetu watu wa filamu tukishindwa kuuza filamu katika Dvd tutafanya nini
ili maisha yaendelee? Maana siku hizi hakuna tena maigizo ya jukwaani
kama zamani na tunahitaji sana sanaa ya maigizo katika majukwaa ni
muhimu
Inawezekana maneno yao yakawa sahihi au si sahihi, kutokana na hali halisi ya mfumo wa tasnia ya filamu ulivyo hasa katika idara ya mauzo, sasa kila mtu anajaribu kutafuta sehemu gani ya kuangukia ndio tunasikia wakisema kuwa toka kifo cha Kanumba hakuna mauzo ya filamu.