Mkurugenzi
wa Kampuni ya Mabasi ya Alsaed, Omary Al Saed wa mjini Morogoro
anakusudia kuwasiliana na wadau wenzake ili kuanzisha Taasisi ya Nasra
Mvungi Foundation, ili kuonyesha namna walivyoguswa na mateso na
hatimaye kifo cha mtoto huyo aliyefichwa kwenye boksi kwa muda wa miaka
mitatu.
Mtoto
huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni mosi mwaka huu, katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa amelezwa
kwa matibabu ya nemonia.Nasra
ambaye kifo chake kimewagusa watu wengi ndani na nje ya Mkoa wa
Morogoro, alizikwa juzi katika makaburi ya Kola mjini hapa.
Akizungumza
na gazeti hilo jana, Al Saed alisema amehuzunishwa na mateso na
hatimaye kifo cha mtoto huyo na kwamba, ili kuonyesha kuwa ameguswa,
ameamua kuwasiliana na wadau wengine ili waone uwezekano wa kuanzisha
mfuko huo.
Alisema mfuko huo pia utatumika kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na wenye mahitaji muhimu.
Alisema hiyo ni njia nzuri ya kukumbuka kifo cha mtoto Nasrah na maisha aliyoishi wakati wa uhai wake.
Mkurugenzi
huyo pia alisema atajenga kaburi la mtoto huyo ili iwe kumbukumbu ya
kudumu kwa watu wa familia yake na jamii kwa ujumla.
Alsaed alisema ujenzi wa kaburi hilo utafanyika mwishoni mwa wiki hii kwa kutumia marumaru.
Wakati
huo huo, Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali mkoani Morogoro, Sunday
Hyera amesema hajui chochote kuhusu namna kesi inayowakabili watu
wanaotuhumiwa kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo itakavyo
kuwa.
Washtakiwa
katika kesi hiyo ni Mariamu Said ambaye ni mama mkubwa wa Nasrah, baba
yake mzazi Rashidi Mvungi na mume wa Mariamu, Omary Mtonga.
Chanzo: Mwananchi.