Mkuu
wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa akionesha
Cocaine zilizokuwa zimefichwa katika mkanda wa suruali aliyokuwa amevaa
raia wa Colombia, Andres Filipe Ballesteros Uribe (28), mara baada ya
kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam.
KIKOSI cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini kinamshikilia Andres Filipe Ballesteros Uribe (28) raia
wa Colombia kwa tuhuma za kuingiza dawa hizo nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini
Dar es Salaam leo, Mkuu wa kikosi hicho, Kamanda Godfrey Nzowa alisema
mtuhumiwa huyo aliingia nchini saa nane usiku kwa ndege ya shirika la
Ethiopian akitokea Adisi Ababa.
Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na Cocaine
iliyofungwa kwenye pakiti sita tofauti na kuiwekasehemu za siri, kiunoni
kama mkanda na nyingine tumboni.Kamanda Nzowa alisema mtuhumiwa huyo
mwenye pasi ya kusafiria namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini
Columbia, alitoka Columbia kupitia Adis Ababa kuja Tanzania huku
akibainisha kwamba hiyo ni njia mpya ya usafirishaji wa dawa hizo
haramu.
“Hawa jamaa wanajaribu kubuni mbinu mpya
kama huyu kijana alikuwa amefunga unga wa cocaine kama zilivyokuwa
zikifungwa pipi na akazimeza… mpaka sasa ameshatoa pipi 13 kwa njia ya
haja kubwa na anaendelea kutoa.
“…Sio rahisi kujua idadi ya mzigo aliokuwa
nao mpaka atakapomaliza kuzitoa zote za tumboni ndiyo tunaweza kusema
uzito wa dawa hizo na thamani yake,” alisema kamanda Nzowa.Alisisitiza
kwamba taarifa sasa wanazopeana kwenye mtandao wao unawezesha kukamatwa
kwa watuhumiwa huku akibainisha kuwa lengo ni kudhibiti usafirishaji kwa
njia yoyote.
Kamanda Nzowa alisema mafanikio yanaonekana
kwa vile kuanzia Juni 24 mwaka huu hadi Agosti 10 hakuna mtu
aliyekamatwa akiingiza huku akibainisha kwamba umadhubuti wa mtandao wao
umefanikisha hilo.
“Asiyeamini kwamba tumefanikiwa atujaribu
aone… naamini tunakokwenda dawa za kulevya hasa cocaine na heroine
zitakuwa hazipiti wala kuingia Tanzania,” alisema na kuongeza kwamba
wanadhibiti pia ulimaji wa bangi.Kwa mujibu wa kamanda huyo lengo la
mtandao wao ni kudhibiti sio kukamata wala kuteketeza.
Picha zote na Francis Dande.