WATU KADHA WANAHOFIWA KUFA MAJI BOTI YA KILIMANJARO II IKITOKEA PEMBA KUJA UNGUJA
Meli ya Kilimanjaro II iliyokumbwa na dharuba katika mkondo wa Nungwi ikitokea Pemba kuja Unguja inahofiwa abiria waliokuwa mbele wamedondoka baharini kati yao saba kati yao hawajulikani waliko.
Meli hiyo ilikumbwa na mawimbi makali katika mkondo huo mapema leo ikiwa na abiria mia nne na 29 wakiwemo watoto 60 na mabaharia wanane.
Akizungumza na Zanzibar Islamic news Blog kamishna wa polisi Zanzibar Hamdan Makame amesema baadhi ya abiria waliokumwemo ndani ya meli hiyo wamelalamika wenzao hawawaoni.
Aidha amesema wamepokea taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazosema watu wanne wameokolewa na wamelazwa katika kituo cha afya Nungwi.
Hata hivyo baadhi ya abiria waliokuwemo ndani ya boti hiyo wamesema mawimbi hayo yamevunja viti vya mbele vya abiria huku baadhi yao wamedondoka baharini.
Waziri wa Miundombinu na Mwasiliano Rashid Seif Suleiman amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kundi la wazamiaji tayari wamekwenda katika eneo la ajali hiyo.
Amwekiri kuwa ni kweli amepokea maelezo kuwa watu saba waliokuwa wakisafiri na chombo hicho wamezama na hawajaonekana.
Waziri Seif amesema kamati ya ulinzi na usalama imekutana mchana huu na kujadili tukio hilo kabla ya kuelekea eneo la tukio kushirikiana na wataalam wengine kuwatafuta watu hao.
Niabu Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai Zanzibar DCI Yussuf Ilembo amesema boti hiyo iliondoka majira ya asubuhi na ilipofika mkondo wa Nungwi ilipigwa wimbi kali na mashine kuzima.
DCI Ilembo amesema abiria waliokuwa wamekaa juu ya boti hiyo waliteleza na kudumbukia baharini wakiwemo watoto, tayari mpango wa kwenda katika eneo la tukio kuwatafuta kwa kushirikiana na wananchi utekelezaji wake umeanza.
Hata hivyo amesema uhakiki wa majina ya wahanga bado unaendelea ili kupata majina yao na umri wao kwa vile kuna meli mbili zilisafiri kwa wakati mmoja.
Kwa upande wake Mkurugenz wa Usafiri wa Baharini (ZMA) Mhandisi Abdi Maalim amesema mabaharia walianza kazi ya kuwatafuta watu wanaosadikiwa kuzama majira ya alasiri leo kwa kushirikiana na mabaharia wa kujitolea.
Afisa mmoja wa kampuni ya Azam Marine amesema chanzo cha tukio hilo ni dhoruba ilioambatana na upepo mkali uliotokea baharini na kuleta taharuki kwa wasafiri.
Wakati chombo kimezimika watu walikata maboya ya uokozi na mtafaruku wa abiria kutaka kujinusuru ulikuwa mkubwa ,chombo hakikuzama ,kimeendelea na safari na kifika katika bandari ya Malindi.
Ajali hiyo ni ya kwanza kutokea mwaka huu ambapo hadi leo alasiri watu walionekana kukaa katika vikundi vikundi na wengine kkufika kwa ajili ya kupokea ndugu zao bila ya kuwaona licha ya meli hiyo kushusha abiria
Wakati huo huo uongozi wa boti hiyo umesema unafanya tathimini ili kujua idadi ya abiria waliodondoka baharini wakati ilipokumbwa na mawimbi.
Nalo Jeshi la polisi Zanzibar kwa kushirikiana na Jeshi la polisi Makao makuu Dar es salaam wametuma helkopta katika eneo la tukio ili kubaini watu ambao wanadaiwa kuzama katika eneo hilo.
Meli hiyo iliwasili bandari ya Malindi majia ya saa 5.00 mchana na iliondoka kisiwani Pemba saa 2.00 asubuhi.
CHANZO:ZANZIBARISLAMICNEWS