Dar
es Salaam. Mkurugenzi wa zamani wa Fedha wa Benki Kuu Tanzania (BoT),
Elisa Issangya amejikuta akitupiwa vyombo vyake nje na Kampuni ya Udalali ya Mwafrika kwa kile kilichoelezwa kutakiwa kuondoka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
Nyumba
hiyo iliyoko Mtaa wa Ruhinde Block 2 Plot 294 eneo la Ada Estate
wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, inaelezwa kuwa inamilikiwa na
BoT. Akizungumza nyumbani kwake baada ya kutupiwa nje vifaa vyake,
Issangya alisema: “Nimeshtukizwa na maofisa wa Kampuni ya Udalali ya
Mwafrika kuingia ndani kwangu na kuniomba nishirikiane nao kutoa vitu
vyangu nje.
“Maofisa
hao wa Kampuni ya Mwafrika walifika nyumbani kwangu asubuhi na
kunionyesha barua kutoka BoT ya kunitaka kuvitoa vyombo vyangu nje,
sikukubaliana nao, nikaamua kwenda polisi kutoa taarifa,” alisema.
Alisema wakiwa polisi na ofisa mmoja wa kampuni hiyo aliyemtaja kwa jina
moja la Gama ambaye alikuwa akimweleza kuwa, watamuelewesha suala hilo
baada ya kuondoa vyombo hivyo , lakini waliporejea nyumbani kwake,
walikuta vyombo vyote vimetupwa nje.
Issangya
alisema kitendo cha kutupiwa vifaa nje ni udhalilishaji kwani
walitakiwa kwenda nyumbani kwake wakiwa na barua ya mahakama ya
kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Nimeshangaa
hatua hiyo wakati mpaka sasa kesi yangu ya kudai haki zangu ipo
mahakamani, wangesubiri mpaka hukumu ikitolewa ndipo waje na uamuzi
huu,” alilalamika Issangya aliyeteuliwa kushika nafasi ya Mkurugenzi wa
Fedha wa BoT mwaka 2000 kabla ya kusimamishwa 2008.
Alipoulzwa
sababu za kufanya hivyo wakati suala la mlalamikaji bado liko katika
vyombo vya sheria na uamuzi wa shauri haujafikiwa, Ofisa wa Kampuni hiyo
ya Udalali, Joseph Gama alisema kuwa wanatekeleza maagizo ya tajiri wao
na si vinginevyo.
“Sisi
tunafanya kazi kwa amri ya tajiri wetu, hatuwezi kufanya mambo kinyume
na maelekezo, tumeelekezwa na huu ni utekelezaji wake,” alisema.
Credit: williammalecela blog