MAFURIKO YAKATA BARABARA RUJEWA NA MADIBIRA MBARALI MBEYA, WANANCHI WAPITA KWENYE MAJI

 Vijana wakivusha mizigo ya wasafiri kutoka Rujewa kuelekea Madibira wilayani Mbarali mkoani Mbeya. 
Barabara hiyo imekatika kwa miezi miwili sasa, baada ya kusombwa na maji. 
Vijana wanavusha mizigo hiyo kwa Sh.1,000-3,000 kwa kila mzigo huku wajawazito, watoto na wazee wakiwa wanapata taabu kuvuka(Picha na Gordon Kalulunga).
 Kulia ni kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail, akiwa na Mwenyekiti wa UVCCM wilayani humo, katika eneo ambalo Barabara ya Rujewa na Ubaruku imekatika.
 Vijana wakivusha mizigo.
  Kushoto ni kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail, akiwa anawasikiliza wakazi wa karibu na eneo hilo ambalo barabara imekatika.
  Kijana Caros, akimweleza kamanda wa UVCCM Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahimu Ismail, jinsi wanavyoshauri Barabara hiyo kujengwa lakini wanapuuzwa na wataalam(wasomi).
 Wakati wengine wanalia, wengine kicheko kwa kuvua samaki aina ya dagaa.....
 Na Gordon Kalulunga, Mbarali

MVUA zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha kukatika mawasiliano ya Barabara inayounganisha eneo la Rujewa na Madibila wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari aliyefika eneo lililoharibika vibaya, baadhi ya wananchi waliokutwa eneo hilo wakivuka ndani ya maji hayo, walisema tangu mwezi Februari mwaka huu eneo hilo halipitiki kwa gari aina yeyote.

Walisema eneo hilo ambalo lipo bondeni, limekuwa korofi kutokana na ukaidi wa wasomi ambao hawataki kusikiliza ushauri wa wenyeji wa maeneo hayo ili kuhamisha barabara hiyo.

‘’Kila mwaka tunawashauri kuwa Barabara hii inapaswa kuhamishiwa upande wa juu, lakini wanakataa na kusema kuwa wakihamisha hawataweza kula pesa kila mwaka ambapo Barabara hii inasombwa na maji’’ alisema mwananchi Caros Elias Mbala.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Mbarali, Amin Kimulungu akiwa sambamba na Kamanda wa UVCCM wilayani humo, Ibrahimu Mwakabwanga, alisema hali ya kukatika mawasiliano ya barabara hiyo imekuwa shida kubwa kwa wananchi wa Madibila, Rujewa na maeneo mengine kila mwaka.

Alisema kinachosikitisha kipande hicho cha barabara kilichosombwa na maji kinatengewa fedha kila mwaka bila kupata ufumbuzi wa kudumu jambo ambalo linakiondolea chama chake heshima ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa mwaka 2005-2010 na 2010-2015.

‘’Maji yote haya yanatoka katika mto wa asili eneo la Ilembula na Malangali Mufindi wilayani Iringa kisha kufurika katika wilaya hii ambayo inategemea maji haya kwa ajili ya kilimo cha Mpunga’’ alisema Kimulungu.

Aliongeza kuwa kuna wakati yeye mwenyewe aliwahi kuhusika kumkodia gari upande wa pili mjamzito mmoja ambaye alizidiwa kutoka Madibila kwenda hospitali ya wilaya Rujewa baada ya kukwama eneo hilo na kutokuwepo na gari ya kuelekea Rujewa.

Kutokana na barabara hiyo kusombwa na maji, bei ya nauli imepanda kutoka Sh 5,000 mpaka 8,000 huku mizigo ikivushwa na vijana kwa Sh 1,000 mpaka 3,000 na shida kubwa ikiwa kwa watoto, wazee na wajawazito ambao hulazimika kukunja nguo zao na kujitosa kwenye maji ili kuvuka upande wa pili na kutafuta usafiri mwingine.

Barabara hiyo inaelezwa kuwa na bajeti ya kiwango cha Lami lakini mpaka sasa utekelezaji wake umebakia mikononi mwa wataalam huku wananchi wakibaki na sintofahamu ya mawasliano ya barabra hiyo.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...