Tembo wakivinjari hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Viongozi
wa makundi ya tembo kati ya 20 na 30 waiishio kwenye ikolojia ya Ruaha
wanatarajiwa kufungwa vifaa maalumu kwa ajili ya kufuatilia nyendo zao
ikiwa ni mkakati wa kuwalinda dhidi ya ujangili.
Ikolojia
ya Ruaha inayojumuisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) ndio yenye
tembo wengi kuliko eneo jingine kwa Tanzania kwa sasa hivyo zinahitajika
juhudi za pamoja katika kuwalinda tembo hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mratibu wa Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao
wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwel Ole
Meing'aki alisema eneo hilo lina tembo wanaofikia 20,090 ambao ni
wengine kuliko eneo jingine.
Mpango
huo utakaotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya
utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta utatekelezwa kupitia
SPANEST ikiwa ni mkakati wa kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.
"Kwa
kawaida tembo huongozwa na jike mkubwa ambaye anajua njia na kuelekeza
kundi zima na ndio watakaofungwa vifaa hivyo. Zoezi hili linahitaji
gharama kubwa kwa kuwa litahusisha wataalamu wengi" alisema.
Alisema
awali Selous ndio iliyokuwa ikiongoza kwa kuwa na makundi makubwa ya
tembo hapo awali lakini kutokana na zoezi la kuhesabu lililofanyika
mwaka jana kwa ufadhili wa mradi huo imebainika kuwa Ruaha inaongoza.
"Kwa
mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Tanzania (TAWIRI) ambao
waliendesha zoezi la kujua idadi ya tembo eneo la Ruaha ni tembo 20,090
waliopo idadi ambayo huenda miaka michache iliyopita ilikuwa zaidi ya
30,000", alisema.
Alisema
tembo hao watafungwa 'Color' ambazo zitakuwa na vifaa maalumu
vitakavyokuwa vikionesha mahali walipo kwa nyakati tofauti.
Alisema
sambamba na kufanya zoezi hilo Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP)
kupitia SPANEST litaimarisha mfumo wa mawasiliano kwenye hifadhi hizo
ili iwe rahisi kwa askari, kituo na kituo kuweza kuwasiliana kwa
urahisi.
Mwenyekiti
wa Mpango wa Matumizi Bora ya Maliasili Idodi na Pawaga (MBOMIPA),
unaojumuisha vijiji vyote vinavyozunguka RUNAPA, Philip Mkumbata alisema
mpango huo ni mzuri na utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili
hasa dhidi ya tembo.