Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu (kulia) akitazama hali
ilivyobaki baada ya bomoabomoa iliyofanywa na Jiji kwenye vibanda vya mamalishe
katika mtaa wa Mbozi, Temeke.
Na Mwandishi Wetu
BOMOA Boboa ya vibanda vya mamalishe katika eneo la Viwanda
la Mbozi, Temeke Dar es Salaam, limezua mtafaruku kufuatia mbunge wa jimbo la
Temeke, Abbas Mtemvu kuwakingia kifua mamalishe hao.
Pamoja na kuahidi kuchukua hatua ya kupambana kisheria na
Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam, inayoendesha bomoa boboa hiyo, Mtemvu
amewata mamalishe kuendelea na shughuli zao katika eneo hilo.
“Jambo hili la kunyanyasa wananchi kwa kuwafukuza katika
maeneo bila kufuata taratibu halikubaliki hata kidogo. Sasa mimi nawasaka watu
hawa wa halimashauri ili kuzungumza nao, lakini wakati nafanyaa hivyo nawaagiza
muwendelee na shughuli zenu hapa, na atakayekuja kuwafukuza mwambieni achukue
kila kitu nami nitapambana naye kisheria”, Mtemvu amesema hayo leo wakati
akizungumza na baadhi ya mamalishe hao katoka eneo la viwanda la Mbozi.
Mtemvu alisema, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck
Sadick na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hawakupaswa kuwafukuza mamalishe
hao kwa kutumia mgambo kuvunja vunja vifaa na kuondoka na baadhi ya vyakula
kama ambavyo imedaiwa, kwa sababu ujenzi wa barabara waliyopo hautarajiwi
kufanywa hivi karibuni.
Amesema mbali na ujenzi wa barabara hiyo ambao Mtemvu
alisema fedha za ujenzi amezitafuta yeye kama mbunge, pia ilipaswa mamalishe
hao kutengenezewa mazingira mengine ya kuendelea na biashara zao kwa kuwa ni
tengemeo kwa wafanyakazi kwenye viwanda vinavyozunguka eneo hilo.
Mtemvu alisema kutimuliwa bila kufanyiwa utaratibu mbadala,
kutawafanya kinana mama, wasichana na vijana wanaojishughulisha na biashara
hiyo ya mamalishe sasa kutafuta njia mbadala ya kuishi hata kama ni haramu
jambo ambalo litakuwa siyo jema kwa taifa.
Juzi, Jiji kwa kutumia mgambo na tingatinga, walivamia eneo
hilo la Mbozi na kusambaratisha vibanda vyote vya mamalishe waliopungua 35, na
inadaiwa kwamba katika operesheni hiyo mgambo waliondoka na baadhi ya vyombo na
vyakula ambavyo hadi sasa havijulikani vilipo.
Mmoja wa Mamalishe eneo la Mtaa wa Viwanda la Mbozi, Temeke
Dar es Salaam, Amina Saidi (kushoto) akilalamika mbele ya Mbunge wa Temeke,
Abbas Mtemvu, mbunge huyo alipotembelea eneo la tukio kuona hali halisi jana
mchana.