MBUNGE wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), amesema heri yeye mwenye mapepo
ya ugomvi wa kupigania masilahi ya wananchi kuliko mapepo ya wizi na
mipasho.
Kauli ya
Mbilinyi maarufu kama Sugu imekuja siku moja baada ya Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Viti
Maalumu, Mary Mwanjelwa (CCM), kumshambulia kwa maneno ya kejeli jimboni
kwake wakidai ana mapepo ya ugomvi.
Waziri Simba
na Mwanjelwa wakiwa katika mkutano wa hadhara katika kata ya Manga,
juzi, walitumia muda mwingi kumchonganisha Sugu na wananchi wake kwamba
anapenda vurugu.
Akijibu hoja
hizo jana kwa simu akiwa nchini China, Sugu alisema yote anayoyafanya
bungeni yana baraka za wananchi wake, ambao walimtuma kupigania maslahi
yao na taifa.
Alisema kazi
yake si kupiga makofi na kuzomea wenzake kama wanavyofanya Simba na
Mwanjelwa wanapokuwa kwenye shughuli za vikao vya Bunge.
“Nawashukuru
wananchi wa Mbeya, maana baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge
niliporudi nyumbani nilipokewa kwa kishindo na kunipa ruhusa ya
kumkabili moja kwa moja Naibu Spika, Job Ndugai, iwapo ataendelea kuleta
uhuni,” alisema.
Huku
akisisitiza kauli hiyo, Sugu alisema utafika wakati atamkabili kiongozi
yeyote atakayeonyesha udhaifu pale anapokalia kiti cha Spika pindi
masuala muhimu ya kitaifa yatakapokuwa yanajadiliwa.
Aliwashangaa
Sofia Simba na Mwanjelwa kumjadili katika jimbo lake na kuyaweka
pembeni matendo yao machafu ambayo wanayafanya bungeni.
Sugu alisema
mmoja wa viongozi hao anasifika kwa udokozi na wizi wa mataulo na
vijiko kwenye hoteli anazofikia na kueleza kwamba hivi karibuni
alisikika katika vyombo vya habari kuwa aliiba vifaa hivyo mkoani
Arusha.
‘Heri mimi
mwenye mapepo ya kupigania masilahi ya taifa bungeni na kama hili la
juzi la muswada wa sheria, kuliko hao wenye mapepo ya udokozi na wizi wa
vifaa vya hotelini.
“Matendo hayo ya udokozi ni kuliaibisha Bunge, wanawake wenzake na chama chake,” alisema.
Alisema kuwa
Mbeya ni mkoa wa wacha Mungu, hivyo haiwapendezi wala hawakubaliani na
mbunge ambaye anapita na kujisifu kwa matendo maovu ukiwamo uzinzi.
Sugu
alimtaka Waziri Simba kutopeleka mipasho kwa wananchi wake, kwa kuwa
hawajazoea mambo hayo na kumtaka kuipeleka kwa wana CCM wenzake.
Aliwataka
wananchi wa Mbeya kutowasikiliza viongozi wachochezi na badala yake
waendelee kupigania maendeleo yao kwa kumtuma kazi ili serikali iweze
kuwajibika kwao.
“Viongozi wa CHADEMA kwao ni kupiga kazi tu, wao wasubiri mwaka 2015,” alisema Sugu.