MSANII
wa muziki wa kizazi kipya, Rehema Chalamila ‘Ray C’ mwishoni mwa wiki
aliandaa sherehe kujipongeza kutimiza mwaka mmoja tangu aanze kutumia
dawa za ‘methadone’ ambazo zimemsaidia kupona uraibu uliotokana na
matumizi ya mihadarati.
Ray C, aliyabainisha hayo Dar es Salaam juzi, alipokuwa akizungumza
na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sigini, alipotembelea Kituo cha Tiba cha Dawa
za Kulevya (Methadone Wing), kilichopo katika hospitali ya Mwananyamala,
Kinondoni.
Alisema ameamua kufanya hivyo kama shukrani zake baada ya kupona
ugonjwa huo, ambao hapo awali ulimfanya apoteze mali nyingi na mwelekeo
wa maisha yake.
“Leo tarehe nane natimiza mwaka tangu nianze kutumia methadone, hivyo
nimeamua kufanya sherehe ndogo na wenzangu ‘rafiki’ katika kituo hiki,
nimenunua vinywaji baridi na vitafunwa kidogo kwa ajili ya kufurahi
pamoja, karibuni sana,” alisema Ray C na kuongeza.
“Sasa najisikia vizuri na namshukuru baba (Rais Kikwete), kwa
kunishauri pamoja na jitihada zake za kuwaleta Wamarekani katika
kutupatia tiba hii ambayo imenirudisha katika hali yangu ya kawaida,
hadi nikaweza kuingia tena studio kurekodi nyimbo tena, ni jambo kubwa
sana na la kujivunia,” alisema Ray C.
Aidha, Ray C aliitaka serikali kuongeza jitihada za mapambano yake,
kwani janga hilo ni kubwa nchini kutokana na ukweli kwamba, wapo hata
baadhi ya vigogo wanaotumia uraibu huo.
Alitoa rai kwa wasanii wenzake, wakiwemo wa filamu na baadhi ya watu
maarufu ambao wamekwishaathirika na wanataabika na maumivu, wasione haya
wajitokeze katika kituo hicho, kwani dawa ya methadone inaponesha.
Aidha, aliwaasa viongozi mbalimbali nchini kuunga mkono juhudi za
Rais Jakaya Kikwete za kupambana na kutokomeza janga la uingizaji na
utumiaji wa mihadarati kwa vijana.
Naye Katibu Mkuu wa Tamisemi, Sagini, aliiagiza Manispaa ya Kinondoni
kuangalia uwezekano wa kuwapatia ajira baadhi ya vijana hao waliopona
kutokana na elimu waliyonayo, kwani katika kundi hilo walikuwepo hata
wasomi wa elimu ya ngazi ya chuo.
Naye mtaalamu katika kitengo hicho, Dk. Elias Mrita, alisema hadi
sasa kuna wagonjwa 375 ambao hupatiwa matibabu na wapo ambao tayari
wamekwishapona, na kwamba kituo hicho kinaendeshwa kwa msaada wa
Serikali ya Marekani.