ABIRIA WANUSURIKA VIFO KATIKA AJALI ZA MABASI YA SUMRY NA NGANGA...

Watu  29 wamejeruhiwa  katika ajali mbili tofauti zilizotokea katika barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam kwenye maeneo ya Mikese na Mkambalani, mkoani hapa. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alithibitisha kutokea kwa ajali hizo na kusema  zilihusisha mabasi ya abiria; moja likiwa basi la Nganga lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na la  Sumry lililokuwa likitoka Tunduma. 
Ajali ya kwanza ambayo majeruhi ni 15 saa 2:30 usiku,  ilitokea juzi eneo la Mkambalani, Morogoro Vijijini.
Ilihusisha basi la kampuni ya Sumry yenye namba za usajili T 888 BWK . Ilikuwa ikiendeshwa na Muhina Mohamedi (39) mkazi wa Mbeya ikitoka Tunduma kwenda Dar es Salaam. 
Basi hilo liligongana uso kwa uso na basi dogo la abiria aina ya Coaster  yenye namba za usajili T273 CCV ambayo dereva wake hakufahamika. Ilikuwa ikitoka Dar es  Salaam kwenda Mbeya. 
Chanzo cha ajali kilitokana na basi la Sumry kutaka kupita gari la mbele yake.
Kwa upande wa ajali ya basi la Nganga lenye namba za usajili T252 AZU, ilikuwa ikiendeshwa  na Alex Eliya (49) mkazi wa Misufini mkoani  kabla ya kupasuka tairi la mbele kulia na kupoteza mwelekeo kisha kupinduka. 
Idadi ya majeruhi katika ajali hiyo ni 14 ambao walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Ajali hiyo ilitokea jana saa 3:30  asubuhi katika eneo la Miembeni Mikese, Wilaya ya Morogoro. 
Baadhi ya majeruhi wa ajali hizo, akiwemo Esau John na Jane Lawa waliokuwa kwenye  basi hilo la Nganga, walisema kilichosaidia kutokuwepo vifo ni kwa kuwa basi halikuwa kwenye mwendo wa kasi. 
Mganga wa zamu katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Alex Makala, alisema jana walibaki majeruhi 12 baada ya wengine kutibiwa na kuruhusiwa kutokana na kuwa na majeraha madogo.


Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...