Waasi wanne wa Ukraine wanaoiunga mkono Urusi wakiwa eneo la ajali. Waasi hao ndiyo wanaodaiwa kuilipua ndege hiyo.
MAMLAKA
nchini Uholanzi imesema kuwa watu 154 raia wa Uholanzi, 27 wa Australia
na tisa wa Uingereza walikuwa miongoni mwa watu 298 waliopoteza maisha
katika ndege ya shirika la Malaysia aina ya Boeing 777-200 yenye namba
MH17 iliyolipuliwa mashariki mwa Ukraine jana.
Maafisa
nchini Ukraine wamesema ndege hiyo ya abiria iliyokuwa ikisafiri kutoka
Amsterdam kuelekea Kualar Lumpur ilidunguliwa katika eneo la mashariki
mwa taifa hilo kwenye kijiji cha Grabovo kilichopo maili 30 kutoka mpaka
wa Urusi na Ukraine ambako waasi wanaoiunga mkono Urusi wamekuwa
wakipigana na vikosi vya serikali.
Rais wa
Ukraine Petro Poroshenko amelitaja tukio hilo kama kitendo cha ugaidi
huku Rais wa Urusi Vladimir Putin akiishutumu Ukraine kwa kutodumisha
amani nchini mwake.
Maafisa
wa Ukraine walichapisha kile walichotaja kuwa mawasiliano ya simu
yaliyonaswa kati ya waasi wakiwaeleza maafisa wa Urusi kwamba ni wao
ndio waliohusika katika kuindungua ndege hiyo.
Waziri wa
mashauri ya nchi za kigeni wa Ukraine, Pavlo Klimkin, amesema kuwa
serikali ina ushahidi wa kutosha kwamba ndege hiyo ilidunguliwa.
Tukio
hili limetokea ikiwa ni miezi minne tangu ndege nyingine ya shirika hilo
la Malaysia kupotelewa ndege aina ya Boeing 777-200ER iliyokuwa na
namba MH370 ikiwa na watu 239 kutoka mataifa 14 ambayo mpaka sasa bado
haijulikani ilipo.